HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUHITIMISHA MKUTANO WA NNE WA BUNGE LA KUMI NA MOJA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 16 SEPTEMBA 2016, DODOMA
    UTANGULIZI        1.  Mheshimiwa Spika,   awali ya yote, naomba kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa  kutulinda na kutupa afya njema hadi kutufikisha siku ya leo  tunapohitimisha Mkutano wa Nne wa Bunge lako Tukufu tuliouanza tarehe 6  Septemba, 2016.      2.  Nitumie  fursa hii pia kukupa pole, Mheshimiwa Spika, kwa maradhi yaliyokusibu  lakini kikubwa nielezee furaha yangu kwa uponyaji ambao Mwenyezi Mungu  amekujalia na hivi sasa tuko pamoja humu ndani. Tunakuombea kwa Mwenyezi  Mungu uendelee kupata nguvu na afya njema.      3.  Mheshimiwa Spika,   tangu tulipokutana mara ya mwisho, kumekuwepo majanga na matukio  mbalimbali ya maradhi, ajali, ujambazi na matukio mengine ambayo  yamesababisha vifo na majeruhi kwa Watanzania wenzetu, wakiwemo  Waheshimiwa Wabunge. Hivyo, ninatoa pole kwa wafiwa wote na wale wote  waliopatwa na majanga kutokana na matukio hayo.  Tunawaombea afya njema wale waliopata majeraha na waliopo hospitali.        4.  Mheshimiwa Spika,  leo tunahi...