HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUHITIMISHA MKUTANO WA NNE WA BUNGE LA KUMI NA MOJA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 16 SEPTEMBA 2016, DODOMA
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika,
awali ya yote, naomba kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kutulinda na kutupa afya njema hadi kutufikisha siku ya leo
tunapohitimisha Mkutano wa Nne wa Bunge lako Tukufu tuliouanza tarehe 6
Septemba, 2016.
2. Nitumie
fursa hii pia kukupa pole, Mheshimiwa Spika, kwa maradhi yaliyokusibu
lakini kikubwa nielezee furaha yangu kwa uponyaji ambao Mwenyezi Mungu
amekujalia na hivi sasa tuko pamoja humu ndani. Tunakuombea kwa Mwenyezi
Mungu uendelee kupata nguvu na afya njema.
3. Mheshimiwa Spika,
tangu tulipokutana mara ya mwisho, kumekuwepo majanga na matukio
mbalimbali ya maradhi, ajali, ujambazi na matukio mengine ambayo
yamesababisha vifo na majeruhi kwa Watanzania wenzetu, wakiwemo
Waheshimiwa Wabunge. Hivyo, ninatoa pole kwa wafiwa wote na wale wote
waliopatwa na majanga kutokana na matukio hayo. Tunawaombea afya njema wale waliopata majeraha na waliopo hospitali.
4. Mheshimiwa Spika, leo tunahitimisha mkutano huu tukiwa tumekamilisha shughuli zote zilizopangwa
kwenye Mkutano huu. Naomba nitumie fursa hii ya awali kabisa
kukupongeza sana Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa
Wenyeviti na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kukamilisha kazi zote kwa
ufanisi mkubwa. Kazi hizo zilijumuisha kujadili na hatimaye kupitisha
Miswada mbalimbali ya Serikali. Napenda kukiri kwamba mijadala ya
mkutano huu ilikuwa ya uwazi na hoja zilizotolewa zililenga kuiletea
maendeleo nchi yetu. Kutokana na michango mizuri ya Waheshimiwa Wabunge
na yenye tija, ilibidi mara kadhaa vikao vyetu kuendelea hadi usiku nje
ya muda wa kikanuni. Nawapongeza sana!
TUKIO LA JANGA LA TETEMEKO LA ARDHI LILILOTOKEA MIKOA YA KANDA YA ZIWA
5. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka kuwa tarehe
13 Septemba, 2016 Serikali iliwasilisha hapa Bungeni taarifa ya
masikitiko kuhusu maafa makubwa yaliyoikumba Nchi yetu tarehe 10
Septemba, 2016 kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea katika Mikoa ya
Kanda ya Ziwa ya Kagera, Geita, Mwanza na Mara. Tukio
hilo ambalo liliathiri zaidi Mkoa wa Kagera lilitokea siku ya Jumamosi
majira ya saa 9.27 alasiri, ambapo Mji wa Bukoba ulikumbwa na tetemeko
la ardhi, lenye nguvu ya mtetemo wa kipimo cha 5.7, kwa kutumia skeli ya
“Ritcher”. Tetemeko hilo limesababisha vifo vya watu 17 na majeruhi 253.
Napenda nitumie nafasi hii kwa mara nyingine kuwapa pole wafiwa wote na
wale waliopata majeraha mbalimbali. Tunaomba Mungu aziweke roho za
Marehemu mahali pema peponi. Amina. Kwa wale waliopata majeraha,
tunamuomba Mungu awaponye haraka.
6. Mheshimiwa Spika,
tukio hilo limesababisha uharibifu mkubwa sana wa nyumba, vituo vya
afya, shule pamoja na miundombinu ya barabara. Aidha, shule nne
za Nyakato, Ihungo, Kashenge na Buhembe, zimeharibika ikiwemo vyoo,
nyumba za walimu, kumbi za shule na mabweni. Nyumba 840 zimeteketea
kabisa, na nyingine 1,264 kupata nyufa. Kwa sasa uongozi wa Mkoa wa Kagera pamoja na Kamati
ya Maafa ya Mkoa na Wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, wataalamu wa
masuala ya matetemeko, na wadau wengine wanaendelea kufanya tathmini ya
kina ya kiasi cha hasara iliyopatikana.
7. Mheshimiwa Spika,
kama Bunge lako Tukufu lilivyojulishwa, Serikali kwa kushirikiana na
Wadau mbalimbali, imechukua hatua kadhaa kushughulikia athari za
tetemeko hilo ikiwa ni pamoja na kufanya jitihada ya kurejesha hali ya
utulivu, miundombinu iliyoharibika ili kuirejesha katika hali ya
kawaida.
8. Mheshimiwa Spika,
pamoja na jitihada mbalimbali zilizofanyika ikiwemo viongozi kutembelea
maeneo yenye madhara, mpaka sasa Serikali imefanya mambo yafuatayo:-
(a) Kuhusu Chakula:
Wananchi wenye mahitaji ya chakula wameendelea kupatiwa chakula kama
vile, unga, mchele na maharage, sukari na chumvi pamoja na mafuta ya
kula. Tathmini ya kubaini mahitaji halisi ya chakula inaendelea.
(b) Kuhusu Matibabu: Serikali
imeimarisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera kwa kupeleka dawa na
vifaa tiba kupitia Bohari Kuu ya Dawa. Aidha, Timu ya Wataalam na
Madakta 12 wamepelekwa Bukoba kutoka Hospitali ya rufaa ya Kanda ya
Bugando. Napenda kuwashukuru pia wadau mbalimbali ambao wamechangia eneo
hili wakiwemo Medecins Sans Frontiers, Ubalozi wa China, Jhpiego (USAID) na Chama cha Wafamasia.
(c) Makazi:
Wananchi waliokosa kabisa hifadhi ya makazi wamepewa maturubai na
mahema kwa ajili ya makazi ya muda. Aidha, waathirika ambao nyumba zao
zimebomoka kabisa, kwa kuanzia kila mmoja ametengewa mabati 20, saruji
mifuko mitano, blanketi na mikeka. Pia wapangaji waliokuwa katika nyumba
hizo kila mmoja ametengewa kodi ya pango ya miezi sita ili apate mahali
pa kujihifadhi.
(d) Kuhusu Shule zilizoathirika:
Serikali inajenga miundombinu ya muda ya shule kama vile madarasa,
mabweni na vyoo hususani katika shule za sekondari za Ihungo na Nyakato
zilizofungwa kwa muda wa wiki mbili. Tathmini ya kitaalam ikikamilika,
mpango wa ujenzi wa miundombinu ya kudumu itafanyika na maandalizi
yanaendelea kupata rasilmali kwa ajili hiyo.
(e) Mazishi:
Serikali imeshiriki katika kuwafariji wafiwa na pia kushiriki mazishi
kwa kusaidia kutoa jeneza, sanda, usafiri na kutenga fedha shilingi
milioni 20 za rambirambi kwa wafiwa ambazo zitatolewa kwao muda wowote
kuanzia sasa.
(f) Barabara:
Tathmini ya uharibifu wa barabara imefanyika na barabara zilizoharibika
zitarejeshwa katika hali ya kawaida ili wananchi waendelee kupata
huduma za msingi. Vilevile, Serikali inaendelea kuchukua hatua za
kuhakikisha miundombinu ya maji safi na maji taka inakarabatiwa na
kuhakikisha usafi unaendelea kuwa katika viwango stahiki.
Kwa
ujumla, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa taasisi za umma ikiwemo
majeshi ya ulinzi na usalama na rasilimali zake vinatumika kutoa huduma
zote muhimu kwa waathirika katika kipindi hiki.
9. Mheshimiwa Spika, hivi sasa
Serikali inaendelea kufanya tathmini ya kitaalam kupitia Wizara ya
Nishati na Madini, Chuo cha Madini Dodoma na Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam kubaini chanzo cha tukio, kiasi cha athari zilizotokea chini ya
miamba na juu ya ardhi. Tathmini hii ya kitaalamu itatupa picha na
mwelekeo wa kushughulikia urejeshaji wa miundombinu iliyoharibika.
10. Mheshimiwa Spika,
naomba nitumie nafasi hii kukushukuru sana wewe binafsi Mheshimiwa
Spika, Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge kwa namna mlivyoshirikiana na
Serikali katika kushughulikia janga hili la kitaifa la tetemeko la ardhi
Napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu ya hali na
mali na kwa kututia moyo katika kushughulikia tukio hili kubwa
lililoathiri maisha na shughuli za wananchi pale mkoani Kagera.
11. Mheshimiwa Spika,
vilevile, kwa niaba ya Serikali, na kipekee, nitumie fursa hii
kuishukuru Jumuiya ya Wafanyabiashara Nchini, Waheshimiwa Mabalozi,
Wawakilishi wa Mashirika ya Umma na ya Kimataifa waliopo nchini,
viongozi wa vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla, ambao waliitikia
wito wa Serikali wa kushiriki na kusaidia juhudi za Serikali za
kuwasaidia waaathirika wa tetemeke la ardhi. Tunawashukuru sana wote
waliotuunga mkono kwa fedha na vifaa mbalimbali.
12. Mheshimiwa Spika,
pamoja na jitihada hizo zinazofanywa, Serikali imeshatoa na inaendelea
kukusanya michango kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali. Hivyo,
kwa wananchi na wadau walio tayari kuchangia wanaweza kutumia Akaunti
ya Maafa iliyofunguliwa katika Benki ya CRDB yenye Namba. 015 222 561 7300 kwa jina la KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode: CORUtztz kwa kutuma fedha kwa njia ya kawaida au Mobile Banking. Vilevile, michango hiyo inaweza kutumwa kwenye Namba za simu za mkononi, 0768-196-669 (M-Pesa), au Namba 0682-950-009 (Airtel Money) au Namba 0718-069-616 (Tigo Pesa).
Nawaomba
wananchi wote, Sekta Binafsi na Jumuiya ya Kimataifa tuonyeshe
mshikamano kuungana na Serikali katika kusaidia wenzetu walioathirika na
tetemeko hilo kwa kutoa michango ya hali na mali.
13. Mheshimiwa Spika,
nitumie fursa hii kuwahakikishia Watanzania wote kuwa Serikali
itaendelea kuratibu michango yote itakayotolewa na kuifikisha kwa
walengwa. Aidha, Serikali itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya
Kimataifa kuimarisha uwezo wetu wa ndani wa kukabiliana na majanga ya
aina hii na mengineyo.
SHUGHULI ZA BUNGE
14. Mheshimiwa Spika, tunahitimisha
mkutano huu tukiwa tumepata fursa ya kujadili Miswada, Maazimio na
Kauli mbalimbali za Mawaziri. Miswada iliyowasilishwa na Serikali na
kusomwa kwa mara ya pili na pia kusomwa mara ya tatu ni kama ifuatavyo:-
Kwanza: Muswada wa Sheria ya upatikanaji wa Habari wa mwaka 2016; (The Access to Information Bill, 2016);
Pili: Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016; (The Valuation and Valuers Registration Bill, 2016);
Tatu: Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa mwaka 2016; (The Government Chemist Laboratory Authority Bill, 2016);
Nne: Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma wa Kemia wa Mwaka 2016; (The Chemist Professionals Bill, 2016);
Tano: Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo wa Mwaka 2016; (The Tanzania Agricultural Research Institute Bill, 2016);
Sita: Muswada wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi wa Mwaka 2016; (The Tanzania Fisheries Research Institute Bill, 2016).
Miswada ya Sheria ya Serikali iliyosomwa kwa mara ya kwanza ni:-
(a) Muswada wa Sheria ya huduma za Hbari za Mwaka 2016 (The Media services Bill, 2016).
(b) Muswada wa Sheria ya marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2016 (The Written Laws Micellianeous Amendments (No.3) Bill, 2016).
15. Mheshimiwa Spika, katika Bunge hili, Serikali ilitoa kauli zifuatazo:-
Kwanza: Kauli
ya Serikali kuhusu hali ya chakula nchini na uzalishaji kwa msimu wa
mazao kwa mwaka 2015/2016; na upatikanaji wa chakula kwa mwaka
2016/2017;
Pili: Kauli
ya Serikali kuhusu tukio la tetemeko la ardhi lililotokea tarehe 10
Septemba, 2016 mkoani Kagera na mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa.
16. Mheshimiwa Spika, kipekee,
naomba kutumia fursa hii kumshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
pamoja na Wataalam wake, kwa mchango wao mkubwa katika kuandaa miswada
hiyo kwa umakini mkubwa na hivyo kuwawezesha Waheshimiwa Mawaziri
kuiwasilisha Bungeni kwa weledi mkubwa. Aidha, napenda kutumia fursa hii
kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri. Serikali
itazingatia ushauri na maoni yenu wakati wa utekelezaji.
17. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu jumla ya maswali 110 ya msingi na mengine 262 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Vilevile, jumla ya maswali matano ya msingi na ya nyongeza ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu ya kila Alhamisi yaliulizwa na kupata majibu.
MWENENDO NA MWELEKEO WA HALI YA UCHUMI
18. Mheshimiwa Spika, katika
siku za hivi karibuni, kumekuwepo na wasiwasi kuhusu mwenendo wa hali
ya uchumi, hususan mtiririko wa fedha kwenye uchumi wa Taifa. Napenda
kutumia fursa hii kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa
ujumla kuwa mwenendo wa uchumi ni wa kuridhisha na unaendelea kuimarika.
Aidha, tathmini iliyofanyika kuhusu viashiria vya uimara wa sekta ya
fedha, inaonesha kuwa Mabenki yetu bado yapo salama, na yana mitaji ya kutosha na mwenendo wa sekta ya fedha ni wa kuridhisha. Aidha,
Wizara ya Fedha na Mipango, Benki Kuu ya Tanzania na Taasisi ya Taifa
ya Takwimu zinafuatilia kwa karibu kuhusu mwenendo wa Hali ya Uchumi
Nchini. Mathalan, tarehe 14 Septemba, 2016 Gavana wa Benki Kuu ya
Tanzania, Profesa Benno Ndulu, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari
kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi nchini ambapo alilihakikishia Taifa na
Jumuiya ya Kimataifa kwamba hali ya uchumi wetu ni shwari kabisa na si
mbaya kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.
19. Mheshimiwa Spika, katika taarifa hiyo ya Benki Kuu pamoja na mambo mengine, imebainishwa kwamba katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ukuaji wa uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa wa kuridhisha. Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na asilimia 5.7 kipindi kama hicho mwaka 2015. Ukuaji huo ulitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme, huduma za mawasiliano, utangazaji na huduma ya intaneti; kuongezeka kwa uchimbaji na madini. Shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kasi ya juu katika kipindi hicho ni sekta ya fedha kwa asilimia 13.5, mawasiliano asilimia 13.4 na utawala wa umma asilimia 10.2.
20. Mheshimiwa Spika,
kwa kuzingatia mwenendo huo mzuri wa viashiria vya shughuli za uchumi,
ni dhahiri kwamba mwelekeo wa uchumi katika kipindi kijacho unatoa
matumaini ya uchumi kuendelea kuimarika kama ilivyokadiriwa hapo awali
na kufikiwa kwa lengo la ukuaji wa Pato la Taifa la asilimia 7.2 kwa
mwaka 2016. Hii inachangiwa pia
na ukweli kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga vizuri katika
kuimarisha uchumi endelevu; usimamizi thabiti wa rasilimali za umma; na
ujenzi wa miundombinu bora yenye kuimarisha lengo la kujenga uchumi wa viwanda chini ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
MWENENDO WA UKUSANYAJI WA MAPATO YA SERIKALI KWA MWEZI JULAI NA AGOSTI, 2016
21. Mheshimiwa Spika, Serikali
ya Awamu ya Tano imedhamiria kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa
mapato ya ndani kwa kuchukua hatua mbalimbali. Katika mwaka 2016/17,
mapato ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kupunguza utegemezi
wa kibajeti kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Aidha, Serikali
imeendelea kudhibiti utoaji wa misamaha ya kodi ili kuleta tija kwa
Taifa katika ukusanyaji mapato.
22. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali imelenga kukusanya mapato ya ndani, ikijumuisha mapato ya Halmashauri, ya jumla ya shilingi trilioni 18.46, sawa na asilimia 62.5 ya bajeti yote ya shilingi trilioni 29.5. Takwimu
za mwenendo wa ukusanyaji mapato zinaonesha kuwa katika kipindi cha
kuanzia Julai hadi Agosti, 2016, mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), yalikuwa shilingi trilioni 2.168 ikilinganishwa na makadirio ya kukusanya shilingi trilioni 2.113, sawa na asilimia 103 ya lengo.
Aina
za kodi zilizochangia sana katika ongezeko hilo ni pamoja na Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya mashine
za kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato. Mapato yasiyo ya kodi kwa
kipindi hicho yalikuwa shilingi bilioni 271.1; sawa na asilimia 60 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 448.4. Aidha, mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri yalikuwa Shilingi bilioni 45.4; ikiwa ni asilimia 41 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 110.9. Napenda kutumia fursa hii kuzihimiza Wizara na Halmashauri kuongeza jitihada za ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
23. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua zifuatazo:-
Kwanza: Kuendelea
kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ikiwa ni pamoja na kufanya
ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo ya biashara, viwandani, migodi,
bandarini, kwenye viwanja vya ndege na maeneo ya mipakani ili
kuhakikisha kodi stahiki zinakusanywa;
Pili: Kusimamia
kikamilifu matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki katika
ukusanyaji wa mapato ili kuongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa
mapato;
Tatu: Kuendelea kupanua wigo wa walipa kodi, ikiwa ni pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iweze kuingia katika mfumo wa kodi;
Nne: Kuimarisha ufuatiliaji wa mapato yanayokusanywa na taasisi na mamlaka mbalimbali za Serikali na Halmashauri zote nchini; na
Tano: Kuendelea kuchukua hatua za kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija.
MPANGO WA SERIKALI WA KUHAMIA DODOMA
24. Mheshimiwa Spika,
tarehe 23 Julai, 2016 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa Chama
cha Mapinduzi hapa Dodoma alieleza kuhusu dhamira ya Serikali ya Awamu
ya Tano ya kukamilisha mchakato na ahadi ya Serikali ya kuhamia katika
Mji wa Makao Makuu – Dodoma. Aidha, Mheshimiwa Rais alirejea kauli hiyo
tarehe 25 Julai, 2016 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Nchini
ambayo yalifanyika Kitaifa kwa mara ya kwanza katika Viwanja vya
Mashujaa, mjini Dodoma. Mheshimiwa Rais alisisitiza kuwa anatarajia
kwamba Serikali yake yote itakuwa imehamia Dodoma katika kipindi cha
miaka minne na miezi minne, hadi kufikia mwisho wa mwaka 2020.
25. Mheshimiwa Spika, napenda kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwamba Mpango wa sasa wa Serikali wa kuhamia Dodoma ni mwendelezo wa utekelezaji
wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 iliyozingatia agizo
lililotolewa tarehe 1 Oktoba, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa Chama
cha TANU. Hivyo, hatua zinazochukuliwa sasa na Serikali ya Awamu ya Tano
ni mwendelezo tu
wa utekelezaji wa mipango ya awali iliyokuwa inatekelezwa mwaka hadi
mwaka na Serikali za Awamu zilizopita, kuanzia Awamu ya Kwanza
lilipotolewa tamko hilo mwaka 1973; chini ya Uongozi wa Rais wa Awamu ya Kwanza na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
26. Mheshimiwa Spika, katika
kutekeleza azma hiyo ya Serikali ya Awamu ya Tano, baada ya tamko la
Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli la tarehe 23 Julai 2016,
yafuatayo yamefanyika:
Kwanza: Tarehe
26 Julai, 2016 nilikutana na Viongozi wa Mkoa wa Dodoma (Viongozi wa
Chama na Serikali wa Mkoa na Wilaya, Wazee maarufu, Viongozi wa
Madhehebu ya Dini na Wadau mbalimbali) ili kuwajulisha kuhusu mkakati wa
sasa wa Serikali wa kuhamia Dodoma. Aidha, niliutaka Uongozi wa Mkoa wa
Dodoma kuwasilisha mapendekezo ya mpango kazi wa kutekeleza uamuzi wa
Serikali wa kuhamia Dodoma;
Pili: Katika
kipindi cha siku 14, Uongozi wa Mkoa wa Dodoma uliwasilisha kwangu
Taarifa ya Serikali kuhamia Dodoma kama ilivyokusudiwa. Aidha, tarehe 15
Agosti, 2016 Mkoa uliwasilisha Mpango huo katika Kikao cha Baraza la
Kazi la Mawaziri pamoja na Makatibu Wakuu na kupata ushauri na maoni yao
ya kuuboresha;
Tatu: Serikali
imeunda Kamati Ndogo chini ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA)
kwa lengo la kufanya mapitio ya upatikanaji wa Ofisi na Makazi na
miundombinu muhimu. Kamati hiyo inashirikisha Taasisi mbalimbali za
Serikali zilizopo Dodoma na Kitaifa, zikiwemo TBA, DUWASA, TANROADS,
TEMESA, TANESCO, SUMATRA, TTCL, Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto na
Uokoaji;
Nne: Aidha, Serikali imeunda Kamati ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu ambao wanaratibu zoezi zima na utaratibu wa Serikali kuhamia Dodoma;
Tano: Tarehe
1 Septemba, 2016, Serikali ilikutana na Watendaji Wakuu wa Taasisi za
Fedha, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Sekta
Binafsi zinazohusika na ujenzi wa miundombinu nchini. Lengo la kikao
hicho lilikuwa ni kupata mawazo ya Sekta Binafsi, Taasisi za Fedha na
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kuisaidia Serikali kuboresha mikakati ya
kuhamia Dodoma kwa kuzingatia kuwa Serikali peke yake haiwezi
kukamilisha jambo hili. Katika kikao hiki tumekubaliana kwamba kuanzia
sasa kuwepo na vikao baina ya Makatibu Wakuu na Wadau wa Sekta Binafsi,
angalau mara moja kwa mwezi chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu Kiongozi
na Katibu wa Kamati hiyo akiwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu. Kikao
hicho kitakuwa cha mashauriano na kupeana mrejesho wa utekelezaji wa
azma ya Serikali ya kuhamia Dodoma kwa kuzingatia mchango wa sekta ya
umma na sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi na
kijamii, uwekezaji na uzalishaji biashara na huduma mbalimbali;
Sita: Serikali pia imeunda Kamati Maalum ya Wataalam Washauri itakayoshirikiana na CDA kufanya Mapitio ya Mpango Kamambe (Master Plan)
wa Mji wa Dodoma ili kubaini mahitaji halisi ya sasa na siku zijazo
katika upeo wa miaka 50 na zaidi. Zoezi hili litahitaji ushirikishwaji
mkubwa wa jamii na sekta binafsi. Lengo la Serikali ni kuwa na mji
uliopangwa vizuri na unaozingatia vigezo mbalimbali vya Kimataifa.
27. Mheshimiwa Spika,
napenda kulijulisha Bunge lako tukufu kwamba Serikali ya Awamu ya Tano
inatambua jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali za awamu zilizopita
zilizoongozwa na Chama cha Mapinduzi za kuweka miundombinu mbalimbali
muhimu ya kufanikisha mpango wa Serikali kuhamia Dodoma. Tathmini
iliyofanywa na OWM, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, pamoja na wadau
mbalimbali, inaonyesha kuwa kwa ujumla miundombinu iliyopo Dodoma kwa
sasa ina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya Serikali kuhamia Dodoma kwa
awamu kuanzia mwezi huu wa Septemba, 2016 hadi mwaka 2020.
RATIBA YA SERIKALI KUHAMIA DODOMA
28. Mheshimiwa Spika,
ili kufanikisha azma ya Serikali kuhamia Dodoma, tayari imeandaliwa
ratiba itakayowezesha Serikali kuhamia Dodoma kwa awamu, kuanzia mwezi
Septemba, 2016 hadi mwaka 2020, bila ya kuathiri bajeti yetu ya mwaka
2016/2017 kama ifuatavyo:
Kwanza: Awamu ya Kwanza itakuwa kati ya mwezi Septemba, 2016 na Februari, 2017.
Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote, Makatibu Wakuu wote, Manaibu
Makatibu Wakuu wote watahamia Dodoma katika Awamu ya Kwanza. Aidha, kila
Wizara itatakiwa kuhamisha Watumishi wa Idara moja au mbili, na wakati
huo huo kuendelea kuweka utaratibu wa kupeleka Watumishi wa Idara
nyingine kuhamia Dodoma;
Pili: Awamu ya Pili itakuwa kati ya mwezi Machi 2017 na Agosti 2017.
Kipindi hiki kitawapa fursa watendaji wa wizara mbalimbali kuweka
katika Bajeti zao za mwaka 2017/2018 gharama za kuendelea kuhamisha
watumishi wake kuja Dodoma;
Tatu: Awamu ya Tatu itakuwa kati ya mwezi Septemba 2017 na Februari 2018; ambapo Wizara zitaendelea na uhamishaji wa Watumishi wa Idara zilizo ndani ya Wizara.
Nne: Awamu ya Nne itakuwa kati ya mwezi Machi 2018 na Agosti, 2018; na Awamu ya Tano itakuwa kati ya Mwezi Septemba 2018 hadi Februari, 2020. Katika kipindi hiki cha Awamu ya Tatu na Nne; Wizara zinatakiwa kuendelea kuhamisha watumishi wake.
Tano: Awamu ya Sita, itakuwa kati ya mwezi Machi, 2020 na Juni, 2020
ambapo Ofisi ya Rais ikiongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, watakuwa wanahamia Dodoma.
Nazishauri
Wizara zote kuanzisha mifumo ya utunzaji kumbukumbu wa kielektroniki
badala ya kuhama na mafaili kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma, tunataka
Dodoma iwe ya kielektroniki.
29. Mheshimiwa Spika,
naomba kutumia fursa hii kuwakaribisha wawekezaji mbalimbali wa sekta
binafsi na wadau wa maendeleo wa ndani na nje kuwekeza Dodoma ili
kuboresha zaidi miundombinu iliyopo na kuongeza majengo ya Ofisi na
makazi ya Watumishi kuwekeza katika huduma za afya na elimu, huduma za
kibiashara kama mabenki, maduka makubwa (Shopping Malls)
na masoko, mahoteli na maghala. Aidha, napenda kurejea maelekezo
niliyoyatoa kwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA) na
Mkoa wa Dodoma na Manispaa kuhakikisha kwamba Mji Mkuu wa Dodoma
unaendelezwa kwa kasi ili kupokea watumishi wengi na familia zao pamoja
na sekta binafsi watakaohamia Dodoma.
30. Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kuwa Mkoa wa Dodoma na CDA wahakikishe kuwa pamoja na kuandaa maeneo ya makazi na Ofisi, pia watenge maeneo
maalumu ya huduma muhimu kama vile maeneo kwa ajili ya kituo kikuu cha
biashara, bustani, bandari kavu na kuendelea kuongeza eneo la viwanda na
huduma mbalimbali za kibiashara. Aidha, naagiza Mamlaka za Mipango Miji
Mkoani Dodoma na hasa CDA wahakikishe wanaweka mfumo wa kielektroniki
wa upatikanaji wa viwanja ambao utatambua mahitaji kwa utaratibu wa
wazi, na bila urasimu usio wa
lazima. Vilevile, nashauri Wakazi wa Mkoa wa Dodoma na Sekta binafsi
kutumia fursa hii kujenga nyumba za kuishi za kutosha, nyumba za kulala
wageni na mahoteli ili watumishi na wageni wanapokuja Dodoma wasipate
taabu kutafuta mahali pazuri pa kuishi.
SEKTA YA KILIMO
Hali ya Uzalishaji na Upatikanaji Chakula Nchini:
31. Mheshimiwa Spika,
tathmini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2015/16
iliyofanyika mwezi Juni 2016 inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa utafikia tani 16,172,841. Aidha, Mikoa 11 kati ya 26 ilibainika kuwa na ziada ya chakula, mikoa 12 kuwa na utoshelevu wa chakula na miwili (2) uhaba wa chakula. Kutokana na mahitaji ya chakula kwa mwaka 2016/2017 kuwa tani 13,159,326, nchi itakuwa na utoshelevu wa chakula kwa wa asilimia 123, sawa na ziada ya tani 3,013,515 kwa mazao yote ya chakula.
32. Mheshimiwa Spika,
tathmini hii ilibaini pia kuwa chakula kingi aina ya nafaka kilikuwa
tayari kimesafirishwa nje ya nchi kutokana na nchi jirani kutokuwa na
mavuno mazuri bila kuzingatia kwanza haja ya utoshelevu wa ndani ya
nchi.
Ili
kuhakikisha kuwepo kwa hali ya usalama wa chakula nchini na kuepuka baa
la njaa hapo baadaye, Serikali imeamua kuwa kuanzia tarehe 10 Septemba
2016 sehemu ya ziada ya nafaka ya mahindi na mchele itasafirishwa nje ya
nchi kwa vibali vitakavyotolewa kwa ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na
Uvuvi pekee. Serikali itasimamia ili kusiwe na upungufu wa chakula nchini.
33. Mheshimiwa Spika,
naomba nitumie fursa hii kuwataka Wakuu wa Mikoa yote nchini
kuwahamasisha wakulima na wafanyabiashara kuongeza thamani ya mazao ya
kilimo hususan mahindi na mpunga kwa kuyasindika, kabla ya kusafirisha
nje ya nchi ili yapate bei nzuri zaidi, na pia kuzalisha ajira kwa Watanzania.
Utaratibu wa kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo katika msimu wa 2016/2017:
34. Mheshimiwa Spika,
kuanzia mwaka 2003/2004 hadi mwaka 2015/2016, Serikali imekuwa ikitoa
ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya
chakula, na hususan mahindi, mpunga na mtama. Pia, ruzuku ya pembejeo
hutolewa kwa mazao ya biashara ya korosho, pamba, chai, kahawa na
alizeti. Ruzuku hiyo, imekuwa ikitolewa kwa kutumia mfumo wa vocha na
vikundi vya wakulima kukopeshwa pembejeo hizo kupitia taasisi za fedha
na makampuni ya pembejeo za kilimo. Pamoja na juhudi hizo, kumekuwepo na
changamoto mbalimbali katika kufikia lengo hilo.
35. Mheshimiwa Spika, ili kuongeza ufanisi, katika msimu wa 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 5 kwa ajili ya ruzuku ya viuatilifu vya mazao ya kilimo na shilingi bilioni 25 kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo nyingine za kilimo. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 20 ni za kununua tani 21,892 za mbolea kwa kaya 354,928. Aidha, Serikali italipia asilimia 30 ya bei ya mbolea
kwenye soko, sawa na shilingi 20,000 kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya
kupandia; na shilingi 12,000 kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya kukuzia.
36. Mheshimiwa Spika, ili mbolea hizo ziweze kuwafikia walengwa kwa wakati na kwa bei nafuu, Kampuni ya Mbolea Tanzania itasambaza mbolea katika vituo vyake 29 nchini na kuiuza kwa Mawakala wa Pembejeo za Kilimo kwa shilingi 38,000 kwa mfuko wa kilo 50 kwa mbolea ya kupandia na shilingi 26,000 kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya kukuzia. Ninaziagiza
Halmashauri zote kuhakikisha Mawakala wa Pembejeo wanauza mbolea kwa
bei itakayopangwa. Ni imani yangu kuwa wakulima wengi watatumia fursa
hii ya kupata mbolea ya ruzuku kuendeleza kilimo cha kisasa, chenye tija
na cha kibiashara.
SEKTA YA USHIRIKA
Maboresho katika tasnia ya Ushirika:
37. Mheshimiwa Spika, kwa
muda mrefu sasa ushirika, kama chombo cha kuwaunganisha, kuwapa nguvu
na kuwatetea wanachama wao katika kilimo, ufugaji, uvuvi na tasnia
nyingine, unakabiliwa na changamoto nyingi za usimamizi mbovu,
ubadhirifu na ufujaji mali wa baadhi ya viongozi. Changamoto hizo
zinawaumiza sana wakulima na kuwafanya wakate tamaa katika uzalishaji,
masoko na uendeshaji wa shughuli zao za kiuchumi.
38. Mheshimiwa Spika,
ili kuondokana na changamoto hizo, Serikali itafanya marekebisho
makubwa ndani ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika; iliyo chini ya Wizara ya
Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kuchukua hatua za kinidhamu kwa
watakaobainika kuhusika na ubadhirifu wa mali za ushirika. Aidha, baadhi ya Maafisa Ushirika waliokaa katika kituo kimoja kwa muda mrefu watahamishiwa katika maeneo mengine.
39. Mheshimiwa Spika,
Serikali itafanya marekebisho makubwa kwa Shirika la Ukaguzi wa Vyama
vya Ushirika (COASCO) ambalo limeshindwa kufanya kazi zake kwa weledi.
40. Mheshimiwa Spika, katika kufufua ushirika, Serikali itahuisha
Sera ya Maendeleo ya Ushirika ya mwaka 2002, na kuijengea Tume ya
Maendeleo ya ushirika uwezo wa kuajiri/kuhamishia watendaji katika ofisi
za Mikoa na Halmashauri zote ili kusimamia vyama vya ushirika; kufanya
kaguzi za mara kwa mara, kuondoa tatizo la upotevu wa rasilimali za
vyama; kusimamia upatikanaji wa viongozi wenye sifa na watendaji wenye
weledi wenye kuongoza vyama kwa ufanisi; kupanua wigo wa shughuli
za ushirika katika sekta nyingine za kiuchumi zaidi ya kilimo ili
kuongeza idadi ya vyama vya ushirika nchini na hivyo kuchochea ukuaji wa
kipato kwa wananchi wengi.
SEKTA YA ELIMU
Motisha kwa Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Kata
41. Mheshimiwa Spika, katika
kuhakikisha kuwa kunakuwa na usimamizi mzuri na wa karibu shuleni,
Serikali imeanza kutoa posho ya madaraka kwa Walimu Wakuu, Wakuu wa
Shule na Waratibu Elimu Kata kila mwezi kuanzia mwezi Julai, 2016 ambapo
kiasi cha shilingi bilioni 5.09 kimetolewa.
Aidha, mpango mwingine uliopo ni kuwapatia Waratibu Elimu Kata pikipiki
ili ziwawezeshe katika ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli za kielimu
katika kata zao nchi nzima. Kwa kuanzia, Waratibu Elimu Kata wa Mikoa 7
ambayo ilikuwa na ufaulu wa chini katika matokeo ya kuhitimu darasa la
saba tayari wameshapatiwa jumla ya pikipiki 1,015. Mikoa iliyopatiwa
pikipiki hizi pamoja na idadi ya pikipiki ni kama ifuatavyo: - Dodoma (192); Mara (99), Simiyu (122), Shinyanga (128), Tabora (200), Kigoma (135), Lindi (139). Mikoa iliyobakia itapatiwa pikipiki chini ya programu ya Kukuza Stadi za Kusoma na Kuandika ya LANES (Literacy and Numeracy Education Support Program) pamoja na UNICEF.
Upungufu wa Walimu na Miundombinu
42. Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa upungufu wa walimu, Serikali imeamua walimu wapya
watakaoajiriwa mwaka 2016 wapangwe shuleni moja kwa moja na kwenye
maeneo yenye upungufu mkubwa wa walimu.
Hali ya Madawati
43. Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa tarehe
16 Machi, 2016 Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli – Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania alitoa agizo kwa Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa
ifikapo tarehe 30 Juni, 2016 kusiwepo mwanafunzi anayekaa chini kwa
kukosa dawati.
44. Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais, kufikia mwezi huu wa Septemba madawati 951,610 kwa shule za Msingi yalitengenezwa na hivyo kufikia madawati 3,084,781 sawa na asilimia 94.4. Kwa upande wa shule za sekondari, idadi ya madawati yaliyotengenezwa yamefikia madawati 1,490,488 sawa na asilimia 99.4 na kufanya upungufu kuwa madawati 182,864 kwa shule za Msingi na 8,380 kwa Shule za Sekondari.
Madawati
hayo yanaendelea kutengenezwa na mikoa ambayo haijakamilisha inatakiwa
iwe imekamilisha ifikapo tarehe 30 Septemba, 2016.
MAABARA KATIKA SHULE ZA SEKONDARI
45. Mheshimiwa Spika, mahitaji ya Maabara kwa shule za sekondari ni 10,803. Maabara zilizopo ni 5,756 sawa na asilimia 53.2 ya mahitaji. Upungufu uliopo ni maabara 5,047
ambazo zingine zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Katika mwaka wa
fedha 2016/17, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri imetenga
jumla ya shilingi bilioni 18.876 kwa ajili ya umaliziaji wa maabara 2,135 katika shule za sekondari kwenye Halmashauri mbalimbali nchini. Serikali inaendelea na ujenzi wa jumla ya maabara 290 kupitia mpango wa MMES II katika shule za sekondari 528. Upungufu utakaokuwepo baada ya kukamilika kwa maabara hizi ni maabara 4,807. Serikali itaendelea kubuni mikakati mbalimbali ya kuondoa upungufu huo.
Mitihani ya Elimu ya Msingi
46. Mheshimiwa Spika, mtihani wa kumaliza darasa la saba ulifanyika tarehe 7 hadi 8 Septemba, 2016 nchini kote. Idadi ya watahiniwa 795,761 walisajiliwa
kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2016. Aidha, taarifa
za awali zinaonesha kuwa takriban watahiniwa 789,302
walifanya mtihani huo, sawa na asilimia 99.2 ya waliosajiliwa. Taarifa
rasmi itatolewa baada ya Mikoa na Halmashauri kukamilisha kufanya
mawasilisho ya taarifa kamili ya ufanyikaji wa Mtihani huo.
47. Mheshimiwa Spika,
tafsiri ya idadi ya kubwa ya wanafunzi waliofanya mitihani ya darasa la
saba ni kwamba yapo matarajio kuwa idadi ya wanafunzi watakaoingia
kidato cha kwanza katika mwaka 2017 itakuwa kubwa kuliko nafasi zitakazo
kuwepo mwanzoni mwa mwaka 2017 katika shule za Sekondari ikiwa hali ya
miundombinu itaendelea kuwa kama ilivyo sasa. Hivyo
basi, natoa wito kwa Halmashauri zote nchini zijiandae kuwawezesha
wanafunzi wote watakaofaulu kujiunga na kidato cha kwanza kwa kuongeza
vyumba vya madarasa, madawati, matundu ya vyoo na nyumba za Walimu.
UHAKIKI WA VYETI KWA WATUMISHI
48. Mheshimiwa Spika,
Serikali imeendelea na zoezi la uhakiki wa vyeti vya watumishi ingawa
limeendelea kuleta usumbufu kwa watumishi katika baadhi ya maeneo.
Naagiza kwa Wakurugenzi waandae vituo maalum vilivyo jirani na vituo
vyao vya kazi badala ya kuwakusanya kituo kimoja ili kuwapunguzia adha
na gharama. Halmashauri zote zizingatie agizo hili ili maafisa utumishi
waende kwenye vituo hivyo.
JITIHADA ZA SERIKALI KUIMARISHA USAFIRI WA ANGA
49. Mheshimiwa Spika,
naomba nitumie fursa hii kuzungumzia kidogo kuhusu jitihada za Serikali
za kuimarisha usafiri wa anga hapa nchini kuanzia mwaka 2016/2017
Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea na mpango wake wa kuboresha usafiri
wa anga hapa nchini. Hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kuendelea
kuboresha viwanja vya ndege nchini. Lengo ni kuhakikisha kuwa kila Mkoa
unakuwa na kiwanja cha ndege cha kisasa, chenye ubora unaofaa kutua
ndege.
50. Mheshimiwa Spika,
ili kwenda sambamba na azma ya Serikali kuhamia Dodoma muda mfupi ujao,
kiwanja cha ndege cha Dodoma kimefanyiwa ukarabati mkubwa ili kuweza
kuhudumia ndege zenye uwezo wa kubeba hadi abiria 90. Sambamba
na hatua hizo, Serikali imedhamiria kuimarisha Kampuni ya Ndege
Tanzania (ATCL), ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ndege mpya kwa ajili ya
kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri wa anga kupitia ATCL.
51. Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imenunua ndege mbili (2) aina ya Dash 8-Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja zitakazotumika kutoa huduma za usafiri wa anga kwa soko la ndani na nchi jirani. Ndege hizo zinatarajia kuwasili nchini mwezi huu wa Septemba, 2016. Aidha, taratibu za kununua ndege nyingine mbili zenye ukubwa wa kati (medium haulage aircraft) zitakazokuwa na uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 110 zimeanza. Ndege hizo zitahudumia soko la kikanda.
52. Mheshimiwa Spika,
pamoja na hatua hiyo Serikali imeanza kazi ya kuiunda upya ATCL. Jana
tarehe 15 Septemba, 2016, Mheshimiwa Rais amefanya uteuzi wa Mtendaji
Mkuu mpya wa ATCL. Aidha,
mchakato wa uteuzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo
unakamilishwa. Vilevile, Serikali imegharamia mafunzo ya wataalam
mbalimbali wakiwemo wahandisi watakaohudumia ndege mpya. Hatua hizo
zitasaidia sana kuboresha shirika letu la ndege na usafiri wa aga hapa
nchini katika kipindi kifupi kijacho.
HALI YA AMANI NA UTULIVU NCHINI
53. Mheshimiwa Spika,
katika kipindi hiki Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine
vya ulinzi na usalama vimeendelea kulinda na kudumisha amani na utulivu
uliopo nchini kwa manufaa ya ustawi wa nchi yetu. Usalama wa raia na
mali zao umeendelea kudumishwa kwa kutambua kuwa ni miongoni mwa misingi
mikuu ya ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Kwa namna ya pekee, napenda
kutumia fursa hii kuvipongeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa
kufanya kazi kwa weledi.
54. Mheshimiwa Spika,
ili Jeshi la Polisi liendelee kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali
ya kubaini, kuzuia na kukabiliana na uhalifu Nchini, Serikali itaendelea
kuwajengea uwezo Maafisa, Wakaguzi na Askari na pia kutekeleza mambo
yafuatayo:-
Kwanza: Kutabiri
mwelekeo wa uhalifu kwa kutumia takwimu za uhalifu, kumbukumbu za
uhalifu pamoja na mabadiliko ya uhalifu ili kuweza kutambua maeneo
korofi, wahalifu wanaohusika, mahali walipo na namna ya kukabiliana na
uhalifu huo.
Pili: Kuyatambua maeneo nyeti (hotspots) yenye vivutio vya uhalifu, na kuyapangia ulinzi, misako na doria imara.
Tatu: Kutoa
elimu kwa jamii kuhusu mbinu mbalimbali za kuzuia na kupambana na
uhalifu kwa kutumia vyombo vya habari, mihadhara, mikutano, maonesho na
usambazaji wa machapisho na vipeperushi.
Nne: Kufanya misako na doria mara kwa mara ili kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali nchini.
Tano: Kushirikiana
na wadau wote wa ulinzi na usalama kubadilishana taarifa za
kiintelijensia pamoja na uzoefu katika kuzuia uhalifu kwa kuibua mifumo
mipya na kuboresha ya zamani.
55. Mheshimiwa Spika,
napenda kusisitiza kuwa suala la amani, na usalama na utulivu nchini
halina mbadala. Nawaomba tudumishe hali ya amani na usalama ili
tufanikishe lengo letu la kukuza uchumi na kuondoa umaskini.
MICHEZO
56. Nchi
yetu imeendelea kuwika kimichezo hasa katika soka. Nitumie fursa hii
kuwapongeza wanamichezo wote na hasa vijana wetu wa Serengeti Boys kwa
ushindi wao wa mabao 9-0 dhidi ya Seychelles. Pia timu yetu iliishinda
Afrika Kusini mabao 3-1. Hivi sasa timu yetu inajipanga kupambana na timu ya Congo (DRC) hapo Septemba 18.
HITIMISHO
57. Mheshimiwa Spika, wakati tunahitimisha mkutano huu leo, napenda nitumie nafasi hii kukushukuru wewe binafsi, Mheshimiwa
Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kusimamia vizuri na kwa
weledi mkubwa vikao vyote vya mkutano huu. Niwashukuru tena Waheshimiwa
Wabunge wote kwa michango yenu. Ninashukuru pia Watendaji wa Serikali
kwa kuwasaidia Mawaziri na Naibu Mawaziri katika kujibu maswali na hoja
mbalimbali za Wabunge. Niwashukuru madereva wote kwa kuwaendesha
Mawaziri, Wabunge na Watendaji wote kwa usalama kabisa. Niwashukuru pia
wanahabari wote kwa kuihabarisha jamii juu ya mkutano wetu. Kipekee,
nimshukuru Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashililah na timu yake kwa
kutuwezesha kukamilisha shughuli zote za mkutano huu kwa mafanikio
makubwa.
58. Mheshimiwa Spika,
wakati tunahitimisha mkutano huu leo na kuelekea katika majimbo yetu,
sote tunatambua kuwa msimu wa mvua za vuli na masika unakaribia. Hivyo,
napenda kutumia fursa hii kuziagiza Wizara zinazohusika na usambazaji
wa pembejeo kuhakikisha zinawafikia wakulima kwa wakati na kwa bei
iliyopangwa. Wakuu wa Mikoa na Wilaya wahakikishe kwamba wanasimamia
kikamilifu shughuli za kilimo katika maeneo yao ili kila familia na kaya
ianze maandalizi ya kilimo mapema.
59. Mheshimiwa Spika,
napenda pia kurejea katika kusisitiza kuwa sekta binafsi ndiyo injini
ya kukuza uchumi katika Taifa letu. Hivyo, nichukue fursa hii
kuwahakikishia wafanyabiashara na wenye viwanda na wawekezaji kwa ujumla
kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuwapa ushirikiano wa dhati
ili kuendeleza shughuli zao kama ambavyo wamejipanga. Wafanye shughuli zao bila woga au tashishi yoyote.
60. Mheshimiwa Spika,
mwisho, lakini si kwa umuhimu, nitumie muda huu kumwomba Mwenyezi Mungu
awalinde na awaongoze Waheshimiwa Wabunge wote katika safari ya kurejea
majumbani kwenu.
61. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, napenda kutoa hoja kuwa Bunge lako tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 1 Novemba, 2016, siku ya Jumanne, saa 3:00 asubuhi litakapokutana katika ukumbi huu hapa Dodoma.
62. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
Maoni