KUFANIKIWA KI -UCHUMI KWA NJIA YA MUNGU



SHUKRANI.
Ninamshukuru Mungu kwa kunipa nafasi ya kukufikia mtu wa Mungu kupitia ujumbe huu.
Pia ninamshukuru mke wangu mpendwa Jane Ayoub kwa kunitia hamasa ya kufanya kazi ya Mungu.Pia watoto wangu Bernadetha Ayoub,Bertha Ayoub na Bernice Ayoub,kwa kuniombea na kuvumilia upweke wangu kwao.
Siwezi kusahau watumishi wa Mungu walioandika na kufundisha masomo yanayofanana na somo hili.Nimejifunza mambo mazuri yaliyofanyika msaada kwangu.Nitataja wachache
1.  Text Box: Watumishi wote hawa na wengine wengi Mungu awabariki/aibariki huduma yenu.Dr.Myles Munroe alifariki dunia lakini kazi yake bado inaishi.Dr.Myles Munroe
2.  Pastor Chris Oyakilome (PHD)
3.  Dr.Mensa Otabil
4.  Rev.Primus Muabuzi
5.  Mwl, Christopher Mwakasege
6.  Bishop Augustine Mpemba
7.  Mch.John Mkuwa   
8.  Fredrick Eliakim
9.  July Bosha- Kiongozi na  mlezi wangu Kiroho
Ninakushauri unaposoma kijitabu hiki utulie kwa makini na kutafakari kwa kina.Nukuu zimetoka katika maandiko matakatifu yaani Biblia.Mahali pengine nimenukuu maandiko ya semina na mafundisho kutoka kwa wapakwa Mafuta wa Bwana.Nina imani utabarikiwa.Ayoub JL



Nukuu muhimu
Hakuna tajiri wala maskini wa muda,kila mmoja ana masaa 24 chini ya jua”
“Mafanikio hayana tabia ya kumrukia Mtu”
“ Jinsi ulivyo ni fursa”
“huduma bora kwa wateja ni silaha tosha”
SOMO : KUFANIKIWA KIUCHUMI KWA NJIA YA MUNGU
Suala la mafanikio kwa Mkristo katika kipindi hiki linakumbana na mitazamo mingi inayotofautiana.Baadhi wakidai mafanikio ni kwa ajili ya kundi la waabudu sanamu maarufu kama Freemason.Swali la msingi ni kweli wana wa Mungu hawatakiwi kufanikiwa kiuchumi ?.
Tunatakiwa kukaa na kutafakari kwa kina kama kuna haja ya Wakristo kufanikiwa katika eneo la kiuchumi.Kama haja ipo Je,nini maana ya mafanikio ?.Njia zipi zinaweza kuchangia watu wa Mungu kufanikiwa?
HEBU TUTAFAKARI KIDOGO MAANDIKO HAYA !
·       Fedha ni mali yangu,na dhahabu ni mali yangu,asema BWANA wa majeshi.(Hag 2:8)
·       Utajiri na heshima ,tena utajiri udumuo viko kwangu Mith 8:18-21
·       Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako ,kama vile roho yako ifanikiwavyo.3yoh 2
·       "Bali utamkumbuka Bwana Mungu wako maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri. ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako kama hivi leo." Kumb 8:18
·       Tajiri na maskini hukutana pamoja; Bwana ndiye aliyewaumba wote wawili.Mith 22:2
·       Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mwanzo 1:26
Ukiangalia maandiko hayo machache kwa jicho la kujifunza kuna kitu utakuwa umeanza kugundua.
Nini maana ya mafanikio ?
ü Ni kuishi maisha ya utoshelevu kukiwa na kusudi la Mungu juu ya maisha yako.
ü Kuendelea kupata kibali cha Mungu juu ya maisha yako, Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.Ef 2:10
ü Ni kufurahia Baraka za Mungu hadi kikombe kifurike.
ü Ni kutimiza kusudi la kuumbwa. Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mwanzo 1:26
ü Ni kupata kibali kwa kila jambo unalolifanya,maana mkono wa Bwana upo juu yako.
KUMBUKA KWAMBA MAFANIKIO NI TOFAUTI NA UTAJIRI. Kwa bahati mbaya, unaposema ‘mafanikio’ wengi hufikiria kuhusu ‘utajiri’.  Unaweza kuwa tajiri lakini ukawa bado hujafanikiwa. Kwa kuwa watu wanawaza utajiri kuwa ndio kigezo cha mafanikio hujikuta wakijiingiza kwenye vitendo vya ajabu kwa lengo la kujizolea mali lakini mwisho huwa wanagundua kuwa hawajafanikiwa japo jamii inahisi wamefanikiwa.Fikiria ni wangapi wana utajiri wa vitu lakini hawana hata maisha yenye maana.
NJIA ZA KUPATA MAFANIKIO
Kila kitu katika maisha ya mwanadamu kina njia zake,mfano ukitaka kwenda mbinguni lazima upitie njia ya wokovu.Kadhalika Mafanikio yana njia zake. Kwani mafanikio hayana tabia ya kumrukia Mtu,badala yake yana namna yanavyoweza kupatikana:-Zifuatazo ni baadhi ya njia ambazo mafanikio halali na haramu (bandia) huweza kuja :-
A. NJIA YA KI-MUNGU- ( Kumb 8:17-18,Hag 2:8,Mith 8:18-21)
Hii ni njia iliyokuu na ya uhakika ambayo kila walioitumia hakika wamethibitisha kuwa ni njia nzuri kwa kuwa inadumu milele. Lakini pia waliopata mafanikio kupitia njia hii wana ujasiri wa kusema jinsi walivyopata.KUMB 8:17 Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo.
18 Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo
Fedha ni mali yangu,na dhahabu ni mali yangu,asema BWANA wa majeshi.(Hag 2:8).Mafanikio haya yana sifa zifuatazo:-
v Yanadumu,
v Yanafurahisha,
v Yanakinga,
v Yana mpatia mwana wa Mungu Amani isiyoelezeka.
v Yana mwongezea mwana wa Mungu heshima,ujasiri,unyenyekevu wa kweli.
v Yana patikana kwa njia halali
v Yana elezeka (Yana ushuhuda )
v Chimbuko lake ni mbinguni.
v Hulindwa kwa damu ya Mwanakondoo aliyechinjwa.YESU PEKEE

B. NJIA YA KI-SHETANI ( Lk 4:5-8)
Akampandisha juu,akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja.(Lk 4:5-8),
SIFA ZAKE :-
v Yanapatikana kwa njia haramu.
v Hayadumu
v Yana mwongezea mwenye mafanikio huzuni,hofu,wasiwasi,kiburi,dharau.
v Yana masharti mengi tena ya aibu tupu.Mfano unaambiwa usivae suruali maisha yako yote au umtoe ndugu/mwenzi au mtoto kuwa kuafara.
v Chimbuko lake ni kuzimu na mtawala wake ni Ibilisi na shetani.Hulindwa kwa matambiko na kuabudu sanamu.
C. NJIA YA KI-BINADAMU( Zab127:1-2,Kumb 30:15,Math 16:26
 Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? Math 16 :26.
Hupatikana kwa jitihada za mwanadamu pekee kwa nguvu na akili zake tu.
SIFA ZA MAFANIKO HAYA
v Hupatikana kwa jasho la mtu na nguvu zake.
v Hutawaliwa na ubahiri uliopitiliza.
v Hutawaliwa na wasiwasi.
v Hakuna kinga.
Kwa nini ni hitaji la msingi kufanikiwa? SABABU ZA MAFANIKIO
a)  Kuthamini kazi ya Yesu msalabani,Alikuwa maskini ili sisi tuwe matajiri 2Cor 8:9,Gal 3:13-14,29.
b)  Kupata mahitaji yako binafsi (mema ya nchi) Isa 1:18-19, …riziki za kila namna 2cor 9:8
c)  Kulifanya agano liwe imara Mwanzo 28:19-21       
d)  Kuujenga ufalme- Kumb 8:6-18,Rum 10:14-15,Ef 4:28
e)  Kwa ajili ya kuihuri Injili ya Yesu ( Math 5:14,Lk 5:4-11,Zek 8:23,
KANUNI YA LAZIMA ILI UPATE MAFANIKIO.
Msingi mkubwa wa mafanikio huanzia rohoni (“Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako,kama vile roho yako ifanikiwavyo”3Yoh 1:2).Ni lazima uwe na nguvu ROHONI. Hakuna njia ya mkato kwa mkristo safi ya kufanikiwa katika maisha, isipokuwa ni kwa kuishi ndani ya mpango wa Mungu uliofunuliwa katika Kristo Yesu
MAHITAJI YA LAZIMA ILI UFANIKIWE
Ili mwana wa Mungu aweze kufanikiwa kuna vitu/mambo ya msingi ambayo lazima yazingatiwe na kufanyiwa kazi.Baadhi ya mahitaji hayo ni :-
a)  Uwepo wa Mungu.Kila jambo katika maisha ya mwanadamu linatakiwa kuanzia katika uwepo wa Mungu.Mahali palipo na uwepo wa Mungu kila kitu kinakubalika kwa Mungu.Hebu tuchunguze andiko hili (“Mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kuwa yeye yupo na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao”. Ebr 11:6).Ukichunguza kwa makini utaona kuwa:-
 i) Kila kitu kinatakiwa kuanza kwa kukiri nafasi ya Mungu.
 ii)Tunahitaji kuwa katika nguvu za Mungu au mafuta yake.Ukiwa na kiu ya mafanikio lazima uwe katika nguvu za Ki-Mungu.Adamu alikuwa katika Edeni ndipo alipopewa majukumu.
Kwa nini ?
Mafanikio ni majukumu siyo starehe.Huwezi kupata majukumu bila nguvu.Nguvu zinapatikana katika uwepo wa Mungu.Hakuna kwingine.Ukiishi nje ya uwepo wa Mungu utakuwa nje ya uwepo!!!!!!!.Hivyo tafuta kwanza uwepo wa Mungu kabla ya kukimbilia mali na fedha au huduma kubwa.Math 6:31-33


Text Box: Nguvu zinapatikana katika uwepo wa Mungu.Hakuna kwingine,hakuna njia ya mkato.Tafuta uwepo kwanza
 
b)  Kujenga wazo la mafanikio.
Nini maana ya wazo ?
Wazo ni dhana.Kila kitu katika maisha huanza na wazo.Hii ni hali ya kuwa na shauku ya moyo ambayo hulenga kuamsha ari ya mafanikio.
Kwa nini ninasema kuamsha ari ya mafanikio?.Hii ni kwa sababu mwanadamu alikusudiwa/ aliumbwa katika hali ya mafanikio. Kila kitu huanzia katika wazo .Wazo la mafanikio lipo katika uwepo wa Mungu(ibada).Zab 32:8,Isa 48:17.Wazo litakufanya uwe na nguvu za kutumika.
Anza kufikiri katika mtazamo wenye nguvu.Acha fikra za kinyonge.Fikra za kujiona wewe si chochote,si lolote huwezi.Akina siwezi hawawezi kamwe chukua hatua. ‘Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; na mwanga utaziangazia njia zako’ (Ayubu 22:28).
Text Box: “Ukiwaza Vibaya Utaishi Vibaya,Ukiwaza Vyema Utaishi Vizuri”Acha kulalamika na kuwa na shutumu zisizo na msingi wowote.Acha kulaumu utawala( Serikali).




c)  Raslimali.Tumia raslimali vizuri acha kubweteka wala kukaa bila kufanya kazi. Mungu hubariki kazi siyo mikono na maneno tu.
ü Mazingira yanayokuzunguka.Mazingira ni fursa.
ü Mbegu (Sadaka,Kikumi,Shukrani,Malimbuko,Kutunza wategemezi na kusaidia wategemezi).
ü Marafiki      Mith 1:10,13:20
ü Muda .
Tumia muda wako vizuri.Acha kulala pasipo sababu.Kijana utakuta unalala hadi saa tatu hujaamka.
·       Kumbuka hakuna tajiri wala maskini wa muda wote tuna masaa 24.
·       Jambo linalowezekana leo lisingoje kesho (Kol 4:5,Ef 15:5).
·        Mafundi tumieni muda vizuri.Acheni kusumbua wateja mkifikiri wataendelea kuwepo kwa lugha zenu za njoo kesho utakuta nimemaliza kushona.Kuna siku watakosekana,fanyeni kazi kwa ratiba na mzitimize.
Weka mpangilio wa ratiba yako vizuri usiishi kiholela.Badilika na nenda kwa wakati.Epuka kuchelewa .Ukichelewa dakika tano(5) utakuwa nyuma dakika tano (5) kimaisha.
ü Uaminifu –Uaminifu ni mtaji.Mtu wa Mungu jitahidi kuwa mwaminifu,watu wengi katika shughuli wanazokabidhiwa wamekuwa na tabia ya kuiba,kila wakisimamia kazi lazima ife,tatizo mkono wa kudokoa.Mpendwa kuwa mwaminifu,utafanikiwa tu.
d)  Bidii katika kazi.Fanya kazi kwa bidii mtu wa Mungu,acha uzembe.Panga muda wa kuwa kwenye mtandao na muda wa kazi,siyo kila muda upo hewani unaongea na simu utafikiri Afisa masoko.Acha kulipua kazi ,fanya kazi hadi watu wakutafute usifanye kama unakimbizwa.
e)  Nidhamu ya kazi.
Ø Jali kazi yako,
Ø Waheshimu wateja,
Ø Tumia lugha nzuri.
Ø Jifunze kukaribisha watu na ukarimu
Ø Wafungie bidhaa kwenye mfuko
Ø Fanya usafi mahali pa kazi,na bidhaa zako ziwe safi.
Ø Vaa vizuri na uwe nadhifu (Smart)
Ø Wahi kazini na mapema.
Ø Jitume kazini.
Ø Weka ubunifu katika kazi zako.
f)    Kusudio la mafanikio.
Mungu hana shida ya kukupa mafanikio lakini anaangalia makusudio yako.Je unataka mafanikio ya nini ? Kwa ajili ya nani ? .Kumbuka mafanikio yalenge kumpatia Mungu Utukufu.Acha kuwaza wewe tu.
Wafilipi 4:19 yanatimia kwetu – nayo yanasema hivi;
"Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu".
" …..vyote ni vyenu .. Vile vilivyopo sasa, au vile vitakavyokuwapo; vyote ni vyenu, nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu" (Wakorintho 3:21,22).
g)  Imani –Mwamini Mungu,ishi maisha ya imani. Mwenye haki ataishi kwa imani yake" (Habakuki 2:4)
ü Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Mithali 3:5, 6
ü Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao. Waebrania 11:6
ü Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye. Waebrania 10:38
ü Zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Ef 6:16
ü Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. Mathayo17:20
Mawazo yetu siyo mawazo ya Mungu; njia zetu si njia za Mungu; na mipango yetu si mipango ya Mungu..
NJIA ZA KUFANYA ILI MAFANIKIO YAWEZE KUDUMU
ü Kudumu katika utakatifu (kukaa katika uwepo) Ukiwa katika ibada tengeneza mazingira ya utulivu ili Mungu akituma Malaika kukupa wazo la mafanikio wakute ukiwa katika utayari wa kupokea
ü Kujikabidhi kwa Mungu kikamilifu Isa 1:19.Acha maisha ya mguu mmoja ndani,mwingine nje.Ukiamua kuokoka okoka kweli usifanye uzembe,shika kwa kumaanisha Neno la Mungu.Ukipata mafanikio isiwe sababu ya kuacha wokovu,wala kuanza kuishi maisha ya michanganyo.Kabidhi mafanikio yako kwa Mungu.
ü Kumkubali Mungu aingie katika ufahamu wako “Rum 1:28,.Ukimkubali Mungu katika ufahamu wako yeye atakupa akili za mbinguni na katika mambo yote Zab 111:10,Kumb 4:6,2Tim 2:7
ü Linda moyo(Uzingire moyo kwa damu ya Mwanakondoo)
Kwa kuwa ndiko zitokazo chemichemi za uzima(Mith 4:23).Kazi yoyote atakayokupa Mungu inahitaji kumwagiliwa ili iweze kustawi.Moyo kama haujajeruhiwa uko salama na hivyo unakuwa katika nafasi ya kubarikiwa bila kipingamizi.
ü Kuwa na tabia ya kumtumikia Mungu kwa mali zako zote,akili zako zote na nguvu zako zote.
Mungu anapotuokoa anataka  tumtumikie ipasavyo,kama wewe ni msomi katika eneo fulani tumia elimu uliyonanyo kufanikisha kazi ya Mungu.Usikubali kuona mambo yanakwenda pasipo utaratibu,shauri,elekeza na onesha kwa vitendo.Mungu atakufurahia .Inawezekana wewe ni Afisa Mipango,saidia kuandika mchanganuo ya miradi katika nyumba ya Mungu.
Angalizo .


Text Box: Tafuta kibali kwanza kabla ya kushauri usije ukaonekana unachukua nafasi ya Mchungaji wako maana kuna viongozi wengine wakishauriwa wanaanza kufikiri unataka kuchukua kiti chao
  
Wachungaji na viongozi wengine tumieni watalaamu waliopo makanisani kufanya kazi ya Mungu kwa ubora.Kumbuka waliopewa uwezo wa kuwa na karama/vipawa zaidi ya kimoja ni wachache.Huwezi kuwa hakimu,Mwalimu,Engineer (Mhandisi),Katibu,Kiongozi wa vijana,Kiongozi wa Sifa pekee yako.Tambua hazina zilizofichwa kwa watu uliopewa na Mungu.
Acha kuhofia kiti chako,wengine hawana mpango wa kuwa wachungaji kwa matakwa yao.Katika hili ninashauri upate muda wa kuwaombea ili Mungu akuoneshe hazina zilizomo kwa kila mmoja.
NGUVU YA SADAKA ILI  MAFANIKIO YAWEZE KUSTAWI.
Sadaka ina nguvu kubwa katika mafanikio.Kila aliye na kiu ya kufanikiwa anatakiwa kuwa na tabia ya kutoa maana kanuni ya kupata ni kutoa. “Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu” (2 Wakorintho 9:6-7).
Utoaji wowote wa sadaka na zaka unaofuata kanuni za Ki-Mungu humtajirisha mtoaji,kwani kutoa sadaka ni kupanda mbegu ambapo kuvuna ni lazima (2Cor 9: 6-10).
Mungu alimbariki Ibrahimu na kumtajirisha kwa kupitia Sadaka(Mwanzo 23:15-16).Sadaka hizo ndizo zinazolifanya taifa la Israeli lionekane kuwa tajiri lenye misingi ya uchumi usioyumba na ulio imara.Uchumi ukiwa imara na ukitumika ipasavyo Taifa linaheshimika na kuwa na nguvu katika kila Idara (Elimu,Afya,Maji,Umeme,Nishati,Ulinzi)..
Je wewe unajua nafasi yako kwa Ibrahimu ? “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu;
10 ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.1Petro 2:9-10
Kwa hiyo ilitoka katika imani, iwe kwa njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote; si kwa wale wa torati tu, ila na kwa wale wa imani ya Ibrahimu; aliye baba yetu sisi sote;
17 (kama ilivyoandikwa, Nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi); mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako.Rum 4:16-17

FAIDA ZA UTOAJI
a)  Mafanikio , ”Baraka ya Bwana hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo”. Mith 10 :22”,Mwa 23 :15 -16,8:21-22,9:1-3,Mal 3:10
b)  Utoaji husaidia kutatua matatizo ya Ki-uchumi,.Petro na wenzake walimwazima Yesu Mtumbwi akautumie kwa kazi ya injili na mara alipowarudishia walipata samaki wengi kupita kawaida. Lk 5: 19.
c)  Sadaka huimarisha ulinzi juu ya mali zako. 10 Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.
11 Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema Bwana wa majeshi.
12 Na mataifa yote watawaiteni heri; maana mtakuwa nchi ya kupendeza sana, asema Bwana wa majeshi.
13 Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema Bwana. ?
Mal 3:10-13,2fal 8: 1-6
d)  Afya na uzima wa kimwili .
Mungu alimzuia shetani asiuguse uhai wa Ayubu “………..Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure?
10 Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi.
11 Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.
12 Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana.
 –Ay 2:6_12
Ø Kufufuka kwa Dorkasi kulichangiwa na maisha ya utoaji Mdo9:36-41
e)  Uzima wa milele –Math  25:31-41,Lk 12:41
f)    Humfanya Mungu akukumbuke “Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.”(Mdo 10 :4)
HASARA ZA KUTOTOA SADAKA KWA UAMINIFU NA UKAMILIFU
             i.        Kufilisiwa na Mungu 1sam 2:7,Hag 1:4
           ii.        Kulaaniwa na Mungu   Mal 3:9
         iii.        Kukosa Baraka za Rohoni –Mith 10:22,Mal 3:10
         iv.        Kukosa uzima wa milele ,Math 25:31-46
KWA NINI MUNGU ANATUPA UTAJIRI ,NGUVU,AKILI ,MALI NA FEDHA(MAFANIKIO) ?
1.        Ili Kuimarisha Agano Lake. Kumb 8:17-18. Agano ni makubaliano ya Kimungu kati yake na wanadamu. Ni zaidi ya mkataba kwani mtu mmoja akivunja agano lazima atawajibika. Mungu alifanya agano na Ibrahimu akimwambia kwamba atambariki na uzao wake utakuwa kama mchanga wa baharini. Kwa hiyo Mungu anataka kuimarisha makubaliano yake na watu wake. Sisi ni wana wa Ibrahimu kwa imani. Kwa hiyo Mungu siyo kama mwanadamu ili aseme uongo na hivyo huimarisha agano lake. Na ndiyo maana Wakristo tunapaswa kutembea na agano la Mungu! Siyo kibiblia kidogo mfukoni mwako bali kutembea na ahadi za Mungu.
Hivyo mafanikio uliyonayo/utakayopewa lengo lake ni kuimarisha agano lako na Mungu.Ukiomba Mungu akufanikishe kumbuka kuwa ukipata mafanikio usimwache Mungu bali weka imara agano lako na yeye aliyekupa.
2. Ili Kuvitumia Kwa Mahitaji Yetu Binafsi. 1Timotheo 6:17. Mungu kama Baba yetu na kama Mchungaji Mwema, anajali sana mahitaji yetu na haja zetu au shauku za mioyo yetu. (vitu vitupavyo furaha na kuridhika).
·       Ndio maana hutupa utajiri, ili tufurahie maisha. - Si mapenzi ya Mungu tuwe masikini. Ndio maana Yesu alifanyika maskini (kimwili) ili kwa umaskini wake, (sisi) tupate kuwa matajiri (kimwili)” 2 Kor 8:9 – .Kusudi la Mungu kukufanikisha ni kwa ajili ya kukidhi mahitaji yako na familia pia.
Tumia mali/ukwasi wako kuwafanya wanaokutegemea wafurahie uwepo wako.Nunua chakula kizuri,weka malazi safi,somesha watoto n.k.
·       Ni mapenzi ya Mungu tupate vitu vyote vitakavyotufanya tufurahie maisha yetu duniani. Nyumba nzuri, mavazi mazuri, chakula kizuri, kazi nzuri, magari mazuri, biashara nzuri, mifugo mizuri, mashamba mazuri, mshahara mzuri, n.k.
·       Inapotokea tunakosa mahitaji yetu siyo kitu cha kujivunia kwa sababu siyo mpango wa Mungu tuwe hivyo.
·       Watu wengi wanapokata tamaa ya kutafuta utajiri na mali hufikia mahali wanasema kwamba ‘haya ni mapenzi ya Mungu nisipate kitu’ kauli kama hizi hazina mashiko yoyote katika maandiko. Hii inatokana na ukweli kwamba Mungu tangu zamani alikuwa anawahudumia watu wake katika mahitaji yao.
* Aliwapa chakula miaka 40 Waisrael bila kufanya kufanya kazi yoyote
* Alimpatia Eliya chakula kupitia Kunguru na hata mwanamke wa Sarepta
*   Mungu amepanga kutimiza mahitaji yako binafsi kupitia mali ambayo amekupa.
3. Ili Kuwagawia Wahitaji (Mathayo 25:31-40). Kulingana na fungu hili haimaanishi kwamba Yesu Kristo alihalalisha umaskini! Hebu soma Mk 14:7 ‘maana siku zote mnao maskini.’ Umaskini umegawanyika katika makundi mawili:-
      a) Umaskini wa kawaida- Huyu anao uwezo kidogo wa kufanya shughuli zake za kila siku lakini shughuli zake hizo haziwezi kumsaidia kukithi mahitaji yake. Kwa hiyo lazima anahitaji kusaidiwa ili aondokane na hali hiyo.
Mara nyingi mtu huyu anakosa raslimali za kumfanikisha hivyo anahitaji msaada wa kujikwamua kutoka hali aliyonayo na kufika mahali fulani.Ushauri wa mtu huyu atafute watu walio na maarifa katika eneo husika watamsaidia na kufikia mafanikio.
      b) Ufukara-huyu hawezi kabisa kupata mahitaji yake maalumu. Na fukara wakati mara nyingi siyo kosa lake kwamba kwa nini amekuwa fukara bali ni kwa sababu maalum. (Yaani Sababu za Kimungu kama Yesu alivyosema ‘Maskini mnao tu sikuzote’ lakini pia Mungu Baba alijua kuwa miongoni mwa jamii kutakuwepo na maskini (Walawi 19:10, 23:22, 25:35; kumb. 15:7,8)
Mungu ametupa mali, fedha na utajiri wa namna nyingi ili tuwasaidie wahitaji na masikini, wajane na yatima, wagonjwa na walemavu. Thawabu yake ni kubwa mbele za Mungu, na Mungu ataona sababu ya kukupa tena na kukuzidishia. Tena Mungu atakufanya uwe njia/mkondo wa baraka zake kwa watu wengine. Mdo 20:35.
AINA ZA MATOLEO.
1.  Sadaka Ya Upendo/Dhabihu
Ni sadaka ambayo inathibitisha namna watu wanavyompenda Mungu na kutambua ulinzi wake kwao na kwa namna ambavyo anawapa mahitaji yao ya kila siku. Sadaka hii hutolewa na watu wote kila Ibada. Lakini watu wengi hutoa sadaka hii kwa mazoea tu. hawajui kanuni za kutoa matoleo hayo. Dhabihu 2Kor 9:6-7. Sadaka ya dhabihu haina hesabu toka kwa Mungu, bali kila mtoaji, anaamua mwenyewe atoe kiasi gani.
Utakavyoamua ndivyo utakavyovuna. Ukitoa kidogo,utavuna au utapimiwa kidogo, ukitoa kwa wingi, utapimiwa vingi. Ni uamuzi wako. (Gal 6:7 – 10) Kazi ya Dhabihu: Ni kupima kiwango cha mavuno ya baraka, unayotakiwa kumiminiwa kutoka mbinguni baada ya kutoa zaka. Dhabihu itazuiliwa kukushukia, kama madirisha yako ya mbinguni yamefungwa. Hivyo kutoa dhabihu wakati unamwibia Mungu zaka, haitaleta mavuno unayotarajia. Watu wengi wana tatizo hili. Hutoa sana sadaka, lakini hawatoi zaka . Baraka zao huzuiliwa.
Kwahiyo, ili umiminiwe baraka katika mashamba, mifugo, afya, biashara, baraka ya pesa, kufaulu, ulinzi, fungua kwanza madirisha, si maombi, wala si kwa sadaka, bali ni kwa zaka yako. Baada ya kutoa zaka, dhabihu inaweza kufanya baraka nyingi sana.
Baada ya madirisha kufunguka, ndipo dhabihu yako itaamua, upimiwe kiasi gani, kijiko au kikombe au bakuli au sufuria au karai au ndoo au pipa au sim-tank au container. Baada ya zaka, dhabihu ndiyo inaamua apimiwe chem–chemi au kijito au mto au bwawa au ziwa au bahari, ni uamuzi wako.
Hakikisha unajiwekea malengo maalumu ya kutoa sadaka kwa kila ibada.  LUKA 6:38, 2KOR 9:10-11
2.  Zaka ( Fungu La Kumi): Walawi 27:30-31 Malaki 3:7 – 7
 Zaka ni 10% (asilimia kumi) au 1/10 au sehemu moja kati ya kumi ya baraka yoyote aliyokupa Mungu. Mfano - Ukikamua lita 50 za maziwa ya ngo’mbe kwa wiki, basi lita 5 ni zaka ya Mungu. Mshahara wako, ukiugawa katika sehemu kumi, basi sehemu moja, mpe Mungu kama zaka yako kwake.  (Malaki 3:10)
Kazi ya zaka – ni kufungua madirisha ya mbinguni ili baraka zimiminwe. Zaka haipimi baraka (mavuno) bali inafungua madirisha ya mbinguni ili upimiwe baraka kutoka kwenye matoleo ya sadaka yako baada ya zaka.
Endapo utazidiwa na matumizi, na ikakulazimu kuitumia zaka takatifu ya Mungu, fahamu kwamba, Mungu anakudai. Siku utakapomrudishia, utatakiwa kulipa pamoja na riba, ili zaka yako ikombolewe. Law. 27:31
Kukombolewa maana yake ili iwe zaka takatifu tena ni lazima uiongezee 20% au 1/5 (sehemu ya tano )ya hiyo zaka, iwe kama riba, ndipo Mungu ataipokea kuwa ni zaka takatifu ya Bwana. La sivyo, zaka yako, si kamili, hivyo si takatifu. Kwa hiyo, haitafungua madirisha ya mbinguni.
3.  Limbuko (Malimbuko): Mith 3:9-10
 Limbuko ni zao la kwanza la kazi ya mikono yako. (First Fruits)Mfano:- Kama umefuga kuku 200 wa mayai, mayai 200 ya kwanza, si ya kula wala kuuza, ni ya BWANA. Ndama wa kwanza kuzaliwa ni wa Mungu, mshahara wa kwanza wa ajira yako ni wa Mungu. Mazao ya kwanza ya shamba lako ni ya Bwana.
Kazi ya limbuko, ni kumheshimu Mungu kuwa ndiye chanzo cha baraka zetu na mpaji wa mali zetu. Ukimtambua Mungu hivyo atakubariki zaidi na kukuzidishia.
4.  Sadaka ya Nadhiri
Nadhiri ni matoleo ya hiari ambayo mtu anajifunga mwenyewe kwa Mungu baada ya kutaka Mungu amtendee jambo fulani la msingi kwake. Mara nyingi sana mtu anatoa bila kushurutishwa na mtu yeyote.
Hii inatokana na kwamba lazima uiondoe kwa vyovyote vile. Watu wengi wana matatizo katika maisha yao ambayo wao wenyewe hawajui yametokana na nini! Ni kwa sababu ya muda mrefu kwa kuiondoa. Wanachelewa kuiondoa. Hebu ngoja nifafanue kwa maandiko matakatifu.
KWA NINI TUNATOA LAKINI HATUPOKEI?
Kanuni ya Mungu ni kupokea baada ya kutoa (kupanda na kuvuna). Kuna nyakati tunapanda lakini hatuvuni, Tunatoa lakini hatupokei. Katika hali kama hiyo, tatizo si Mungu, maana “Mungu, si mwanadamu hata aseme uongo” Hesabu 23:19. Bali ni sisi wapandaji/watoaji tunakosea masharti ya kupanda/kutoa.
Mungu anasema katika Yakobo 4:3 “Hata mwaomba, wala hampati, kwasababu mwaomba vibaya”. Basi ni lazima na hakika ya kwamba, “tunatoa lakini hatupokei, ni kwa sababu tunatoa vibaya” !! Yafuatayo ni baadhi ya mambo yanayotufanya tusipokee japo tunatoa.
a)  Kukosa mifereji ya baraka na kuwa na visima vya baraka tu. watu wengi sana wanataka baraka lakini Mungu anapotaka kuwabariki anakosa mahali pa kubariki. Ipo mifano mingi katika Biblia ya watu ambao waliwahi kukaa kwa watu maarufu na wenye fedha kabisa lakini walibaki kama walivyo mpaka hapo walipokuwa wameamua kupata kazi zao.
Mtu wa Mungu jitahidi kuwa na kazi ya kufanya kwa kuwa Mungu hubariki kazi ya mikono yako.
*   Yusufu alipokuwa katika nyumba ya Potifa, nyumba ile ilibarikiwa sana lakini Yusufu hakubarikiwa kwa sababu ile kazi aliyofanya haikuwa yake. Watu wengi hawakumbuki jambo hili kwamba japokuwa wanafanya kazi kwa watu kazi hizo siyo kazi zao!
Kwa mfano wewe ukiwa kama mwalimu-hiyo kazi siyo yako bali ni ya mwajiri wako na ndiyo maana unawajibika kwake. Kwa hiyo lazima ufanye kazi na malengo ili umiliki kazi yako mwenyewe.
*   Yakobo alipokuwa katika nyumba ya Labani, nyumba hiyo ilibarikiwa sana lakini mpaka ilipofika wakati wa kutambua kwamba Mungu hakupanga aishi kwa Labani kwa kipindi hicho. Labani alitaka kumweka Yakobo awe kitega uchumi kwake lakini jamaa huyu alikuwa anajiamini na anamwamini Mungu wake sana. Mwa.30:27-31
*   Tatizo la wapendwa wengi ni kwamba hawana kitu ambacho kwacho Mungu akishuka anataka awabariki sana. Wameweka akiba ya baraka zao kwa Mungu na hivyo Mungu bado amekosa pa kuweka. Hawana kazi zao wenyewe bali wana kazi za mabosi wao tu. Tumia akili yako sawasawa! Hakikisha unamiliki cha kwako huku ukiendelea na kazi nyingine!
b)  Kumwibia Mungu Zaka. (Mal 3:7-12). Kutoa sadaka wakati unamwibia Mungu zaka, hakuna faida, kwa sababu madirisha ya mbinguni yamefungwa. Sadaka haitazaa. Sadaka yako italeta mavuno mazuri endapo tu madirisha yako ya mbinguni yamefunguliwa kwa zaka unayotoa. Usimwibie Mungu. Toa zaka kwa uaminifu. Utaanza kuona unapokea mavuno (baraka) kwa kipimo cha kujaa na kushindiliwa hata kumwagika.
c)  Kutoa sadaka bila imani (Ebr 11:1,6; Ebr 10:38) “Imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo” wengi hutoa sadaka lakini hawana uhakika kuwa ile sadaka itazaa mara 30 au mara 60 au mara 100 (Mathayo 13:3,8)
*   Kwa sababu wengi hutoa bila uhakika (imani) sadaka zao haziwi za kupendeza mbele za Mungu. Hivyo hazizai. Kwa sababu hiyo, wanajikuta wanaamini kwamba, ukitoa sadaka, ni kama wamechanga pesa tu, na haitazamiwi kuzaa. Ni kama imepotea. Hayo ni mawazo potofu ambayo shetani amewafanya wengi kuamini hivyo.
*   Lakini NENO la Mungu linatupa uhakika (imani) kwa kuwa “imani huja kwa kusikia . Neno la Kristo (Rum 10:17). Mtu akiliamini neno la Mungu, kwamba Mungu hawezi kusema uongo, moyo wake utapokea uhakika (imani). Ndani yake, litajengeka taraja la kupokea, kila anapotoa. Atajua kuwa kutoa sadaka si kupoteza, bali ni kupanda kwa ajili ya mavuno (baraka) kubwa zaidi.
Kuanzia sasa, pokea uhakika kwamba, ukitoa kwa imani ya kupokea, utapokea. Ukitoa bila imani ya kupokea, hautapokea, utakuwa umechangia tu . Hivyo mbegu haiwezi kuzaa, kwa maana “….kila tendo isilotoka katika imani, ni dhambi” (Rum 14:23)
*   Hakuna mkulima anayeweza kutoa kidogo, wakati anaamini mavuno ni mengi. Atoae kidogo hana imani ya kupokea. Anaamini “inapotea”na ndio maana anaona ni bora apoteze kidogo.
*   Lakini mwenye imani ya kupokea, hutoa kwa wingi kwa sababu anajua sadaka yake haipotei, bali imepandwa na itazaa sana.3. Kutoa sadaka pungufu ya ile uliyoazimia mwanzo au pungufu ya ile aliyokuongoza Mungu kutoa. (Mdo 5:1-11; Mith 21:27)
*   Ukipanga moyoni mwako kutoka nyumbani, kumpa Mungu kiasi fulani cha sadaka, baada ya azma hiyo, Mungu anakuwa ameipokea sadaka tayari. Wakati wa utoaji, usipunguze. Laa sivyo utakuwa unamwibia Mungu. • Watu wengi hukosea kwa kufika ibadani wakiwa wamepunguza sadaka ya Mungu. Katika sadaka hiyo hiyo ananunua gazeti, pipi, au analipa nauli. Hiyo sadaka si takatifu tena. Kwa sababu umeipunguza.
*   Panga kutoa sadaka kwa maombi kabisa, uamue kiasi utakachomtolea Mungu na uwe mwaninifu kutokuipunguza, hata iweje. Baadhi ya mikosi itupatayo, ni matokeo ya kumwibia Mungu, kama Anania na Safira .

d)  Kutoa sadaka kilema Mal 1:13- 14, Walawi 22:20-25 Sadaka kilema ni ile ambayo hata wewe hauihitaji. Ni zile sadaka tunazotoa ili kupunguza mizigo.
ü Mungu hapokei sadaka zilizokataliwa Kamwe, usitoe mabaki (ya dukani, shambani, nyumbani, n.k.) kuwa sadaka, si heshima! Ni laana mbele za Mungu.
ü Mungu hupokea sadaka nono, sadaka nzuri, sadaka bora. “Mheshimu Mungu kwa matoleo yako” Mith 3:9 Kama ulichotoa, ndicho pekee kulikuwa kimebaki, Mungu atakipokea vizuri na machoni pake kitakuwa “kinono” hata kama ni kichache, kichakavu au kilema, kwa sababu ndicho pekee ulichobakiza.
e)  Kutoa sadaka dhalimu/haramu (Malaki 3:12-13)
*   Sadaka haramu ni ile iliyopatikana kwa udhalimu, kwa mfano; biashara haramu, dhuluma, rushwa, wizi, uuaji, utapeli, uasi n.k. Wewe ufanyaye mambo ya jinsi hii, ni chukizo mbele za Mungu.
*   Sadaka ya namna hii, haitabarikiwa. Ni haramu. Isa 1:11 –17; Amosi 5:22-27.6. Kutoa sadaka bila upendo wa Kristo ndani yako. (1Kor 13:1-4) Kama moyo wako unamchukia mtu, jirani, ndugu, au watu wa dhehebu jingine au kabila jingine, haufai kutoa sadaka. Biblia inasema hakuna faida.Kama umekosana na mtu, yakupasa kutengeneza uhusiano wenu kwanza, kabla ya kutoa sadaka.(Math 5:23-25)
Utoaji ni ibada kamili. Unatakiwa utoe sadaka bila hila, bila kinyongo, bila chuki, bila hasira wala ugomvi au kwazo juu ya mtu. Moyo wako uwe safi. Kama una neno juu ya mtu,Ungamaneni dhambi ninyi kwa ninyi mpate kuponywa.” (Yak 5:16)
*   Upendo wa kweli unaunganishwa na amani ya rohoni (Efe 4:1-3) (Ebr 12:14) Mungu anataka tutafute kwa bidii amani (upendo na umoja) ili tupate na baraka zake maishani. Upendo wa kweli, huleta umoja, ambapo Mungu ameamuru baraka zake. (Zab 133:1-3)
f)    Kutoa sadaka ili usifiwe (Math 6:2-4; Mith 21-27) Maana ya andiko hili, sio sadaka yako kuonekana. Bali ni ile nia ya moyoni. Haimaanishi jirani (mkono) yako akiiona sadaka yako, itakuwa batili. Ila kama uliionyesha au uliitaja ili usifiwe, hapo imekuwa batili. Haitakuja na baraka yoyote.
g)  Kutoa sadaka mahali ambapo hukutakiwa kutoa (Kumb 12:13-14) Kila sadaka (mbegu) ina mahali pake maalum pa kutolewa (kupandwa). Kuna mbegu hazioti vizuri Ulaya, Afrika, milimnani, mabondeni, mchangani, pwani, majini, n.k.

*   Ni muhimu kusikiliza uongozi wa Roho Mtakatifu. Kama sadaka yako Mungu alitaka uitoe kwa yatima, ukiitoa kanisani, utakuwa umekosea. Ni muhimu umuulize Mungu, umsikilize na umtii vizuri. Kuna sadaka za kanisani na za sehemu nyingine nje ya kanisa, kwa mfano; kwa yatima, wajane, masikini, mikutano, semina, safari za watumishi, nyumbani kwa watumishi na Serikalini.
*   Tazama Math 13:1-9. Tatizo halikuwa kwa mpanzi, wala katika mbegu zake, bali katika “mahali” mbegu hizo zilipoangukia.  Si kila udongo, ni udongo tifu-tifu. Udongo tifu-tifu ni pale mahali Roho anakuongoza kutoa. Mahali ambapo kazi ya Mungu inafanyika vizuri kwa utukufu wa Mungu. Mfano:- Kanisani / Mikutanoni, (Mdo 4:36) Wahubiri wa injili (Fil 4:15-20; Gal 6:6). Kwa Maskini, Yatima, Wajane (Mdo 10:1-4,Isa 1:10-17)
*    Roho Mtakatifu na akuongoze (Rum 8:14; Yoh 16:13)9. Kutoa sadaka wakati ambapo hukutakiwa kutoa. (Mhu 3:1-2, 6) Kila jambo lina wakati wake. Hata mbegu, hazipandwi kila siku. Zina majira yake ya kupandwa na kuvunwa. Jifunze kutoa sadaka kwa wakati ambao Mungu anakusukuma kutoa. Msukumo wa Mungu ukija kukugusa kutoa sasa, lakini ukaacha kutii, halafu ukaamua kutoa wiki ijayo, si ajabu usipokee mavuno ya sadaka yako. Kuchelewa kutii ni kutokutii .Huwezi kujua, pengine dakika ile na siku ile, sadaka yako hiyo ilihitajika sana mahali Mungu alipokuwa anakuongoza kutoa. Kwa kutokutii kwako, umekwamisha kazi yake na hutaweza kubarikiwa. (Isa 1:19)
h)  Kutoa sadaka ili kukubaliwa na Mungu. (Mdo10: 1-6)
Kornelio alidhani Mungu atamhesabia haki kwa wingi wa sadaka na sala zake. Lakini Mungu alimhurumia na akamwonyesha namna sahihi ya kuhesabiwa haki. Yaani wokovu kupitia kwa Yesu Kristo.
*   Watu wengi wanatumia sadaka kutafuta haki ya Mungu. Sadaka za hivyo, hazileti baraka. Zinafanana na rushwa. Huwezi kumhonga Mungu kwa pesa au maombi. Haki ya Mungu inapatikana bure, kwa toba ya kweli na wokovu kupitia Yesu Kristo. (Mdo 10:17-48) (Efe 2:8-9).
Toa sadaka kwa moyo safi, kwa nia ya kumwabudu Mungu na kuisukuma injili mbele. Nawe utabarikiwa sana.
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, na upendo wa Mungu Baba na Ushirika wa Roho Mtakatifu, ukae nasi sote, sasa na hata milele. (2Kor13:14) NI BORA KUTOKUTOA KABISA.

TAFAKARI MAMBO HAYA UNAPOTOA SADAKA YAKO
1.  Toa kulingana na jinsi Mungu alivyokubariki.
2.  Toa kwa hiari bila kulazimishwa. Acha kutegemea ushawishi wachungaji makanisani. Kuna watu wengi hawapendi kutoa mpaka hapo wameshawishiwa vya kutosha ndipo watoe. Hii ndiyo sababu makanisa ya uongo yanatumia mbinu hizo lakini kusema kweli ni kwamba tunahitaji kutoa sadaka inayopendeza mbele za Mungu kwa hiari.
3.  Usitoe chochote tu. kuna watu wengine ambao hawachagui sadaka za kutoa. Unaposhindwa kuchagua sadaka za kutoa mbele za Mungu ni dalili ya kushindwa kufanikiwa katika maisha yao. Nafiki kila mtu anapotaka kumpelekea mtu anayempenda kitu anatamani ampelekee kitu kizuri ambacho atafurahi mara baada ya kupokea! Ndiyo hivyo hata Mungu anataka tuchague vitu vizuri vya kumtolea.
4.  Toa kwa furaha. Kuna mtu mwingine anatoa kwa huzuni kweli kweli. Hana furaha moyoni mwake. Anaona ni mzigo mkubwa sana moyoni kutoa sadaka hiyo.  Mimi napenda sana kipindi cha matoleo kwa sababu ni wakati wa kwenda kupanda na kupokea. Lakini kuna watu wengine ukifika wakati wa sadaka kanisani anajisikia haja kubwa na kutoka nje kwenda chooni ili akute wamemaliza kutoa. Kama unaona hivyo ujue kwamba katika eneo la utoaji una matatizo.
5.  Toa kwa imani. Chochote kile unachokitoa unahitaji kukitoa kwa imani kwamba kimepokelewa na Mungu na pia ujue kwamba katika kupanda kwako utavuna kwa wakati wake usipozimia roho yako. Usitoe kwa sababu wanasema utoe! Toa kwa sababu ni wakati wako kwenda kuinua kiwango cha imani yako. Ukiangalia ndani ya kanisa watu ambao wanatoa matoleo kwa imani ndio watu ambao wamebarikiwa san asana.
6.  Toa kila mara. Watu wengine hufikiri kwamba utoaji una mwisho wake. Mwisho wa utoaji kwako ni kifo chako. Kama ukifa leo ndiyo mwisho wako wa kutoa.
7.  Toa sadaka na kuiipa jina. Kila sadaka ina jina lake. Na ndiyo maana katika Biblia kuna sadaka ya amani, malimbuko zaka nk. Kwa hiyo ni vizuri zaidi kuipa jina sadaka yako. Je ni shukrani? Je ni kwa nini unatoa? Ni sadaka ya upendo au? Nk.
8.  Usitoe ili uonekane na watu. Watu wengine hawawezi kutoa sadaka zao wakiwa peke yao. Wanapenda waonekane kwa watu kwamba wanatoa sadaka kubwa! Huo sio utoaji kamili! Wakati mwingine unahitaji kutoa sadaka ya siri badala ya kutangaza tangaza kwa watu. Tamani Mungu akuone katika utoaji wako badala ya watu wakuone katika sadaka hiyo..

 
SOMO HILI LIMEANDALIWA NA,
MWL,AYOUB JACOB LEO
FPCT-KISESA,MWANZA

MAWASILIANO
SIMU : +255 (0) 755 035 722 AU +255 (0) 785 645 177

BARUA PEPE (E-MAIL )
BLOG : www.nsanacz.blogspot.com

Kimeandikwa na kuchapishwa na
Nsana Computing Zone
Stand ya Kwanza Kisesa-Mwanza
S.L.P 2637-MWANZA

BLOG : www.nsanacz.blogspot.com




Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

UCHAMBUZI WA KITABU CHA DANIELI

SOMO: NGUVU YA DAMU YA YESU KATIKA KUWEKA AGANO