Dkt. Akwilapo awataka wahitimu wa ADEM kusimamia kanuni na taratibu katika utendaji kazi.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia Dkt. Leornard Akwilapo amewataka wahitimu wa kozi za
Uongozi na Usimamizi wa Elimu zinazotolewa na Wakala wa Maendeleo ya
Uongozi wa Elimu (ADEM) kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa Sera ya
Elimu na Mafunzo ya mwaka(2014), Sheria, Kanuni na Taratibu za Elimu ili
kupunguza migogoro shuleni
Katibu Mkuu ameyasema hayo katika
mahafali ya Ishirini na tano (25) yaliyofanyika katika Chuo hicho
kilichopo Bagamoyo Mkoani Pwani ambapo amewataka ADEM kuendelea
kusimamia utekelezaji wa Mtaala kwa ufanisi, kutoa takwimu sahihi za
shule, kupanga mipango ya maendeleo ya shule inayotekelezeka, kusimamia
fedha za elimu bila malipo kwa ufanisi.
Eneo lingine ambalo Katibu Mkuu ametaka
litiliwe mkazo ni pamoja na kudhibiti nidhamu za wanafunzi mara
warudipo katika vituo vyao vya kazi.
Dkt. Akwilapo amesema mafunzo ya uongozi
na usimamizi wa Elimu pamoja na Ukaguzi wa Shule ni muhimu katika
kuwapa uwezo walimu na viongozi wa elimu kufanya kazi zao kwa weledi,
ufanisi na kwa kujiamini zaidi hususani katika kipindi hiki cha
maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia.
Amewataka wahitimu kuwa chachu ya
mabadiliko katika Uongozi na Utawala Bora pamoja na Uthibiti Ubora wa
Shule nchini kwa kutumia ujuzi, maarifa, stadi na mbinu mpya
walizozipata katika mafunzo ikiwa ni pamoja na maarifa waliyoyapata
kuyaeneza kwa walimu ambao hawajapata fursa ya kupata mafunzo hayo.
Source
WIZARA YA ELIMU,SAYANSI NA TEKNOLOJIA
24 November 2017
Maoni