taarifa kwa vyombo vya habari
taarifa kwa vyombo vya habari
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu : +255-22-2114512, 2116898
Email : press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz
Faksi : 255-22-2113425
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM,
TANZANIA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Watanzania na taasisi mbalimbali kutumia takwimu sahihi zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na kujiepusha na takwimu za upotoshaji zinazosambazwa na baadhi ya watu kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Mhe. Rais Magufuli amesema hayo tarehe 20 Desemba, 2017 katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu inayojengwa katika eneo la Makulu Mjini Dodoma.
Pamoja na wito huo Mhe. Rais Magufuli ameitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu pamoja na vyombo vingine husika kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu yeyote ama taasisi itakayotoa takwimu za upotoshaji.
“Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania tumieni takwimu sahihi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, puuzeni takwimu za kupika zinazotolewa na baadhi ya watu kwenye mitandao, wapuuzeni hata wanaosema vyuma vimebana, vyuma vimebana kwa wanaotaka vya bure lakini wanaochapa kazi vyuma havijabana” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Amebainisha kuwa uchumi wa Tanzania unakwenda vizuri ambapo katika nusu ya kwanza ya mwaka huu umekua kwa asilimia 6.8, mfumuko wa bei umeshuka hadi asilimia 4.4 kwa mwezi Novemba 2017 na akiba ya fedha za kigeni imefikia Dola za Marekani Bilioni 5.82 ambayo inaiwezesha nchi kununua bidhaa na huduma kwa miezi mitano, ikilinganishwa na wastani unaopaswa wa miezi miezi 4.
Mhe. Rais Magufuli ameongeza kuwa Serikali imeendelea kufanya mambo makubwa ya maendeleo ya nchi ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma utakaogharimu Shilingi Trilioni 7.6, kutoa fedha za dawa ambazo zimeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 31 hadi 269, kutoa Shilingi Bilioni 23.876 kwa ajili ya elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari kila mwezi, mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge), kuongeza mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka Shilingi Bilioni 373 hadi Shilingi Bilioni 483 na mengine mengi.
“Hizi ndio takwimu sahihi, na nyinyi Ofisi ya Taifa ya Takwimu mkiona mtu anapotosha ukweli huu mkamateni mpelekeni mahakamani akajifunze kupata takwimu sahihi”
“Haya tunayoyafanya wale ambao walikuwa wanapata fedha za bure lazima watapiga kelele kuwa vyuma vimebana, lakini tunabana vya bure ili kuwaletea wananchi maendeleo, na kwa kweli tutabana sana” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa na wafanyakazi wote wa ofisi hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya na pia ameishukuru Benki ya Dunia, Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) na Shirika la Maendeleo la Canada kwa ufadhili wake waliowezesha kujengwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mjini Dodoma na Ofisi nyingine iliyojengwa Zanzibar pamoja na kusaidia shughuli nyingine za Ofisi hiyo.
Ujenzi wa jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mjini Dodoma lenye ghorofa nne na ukubwa mita za mraba 7,100 ulianza Machi 2017 na unatarajiwa kukamilika Januari 2018 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 11.6.
Katika taarifa yake kwa Mhe. Rais Magufuli Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa amesema kwa kutambua umuhimu wa takwimu katika kupanga, kutekeleza na kusimamia masuala mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa jamii, ofisi yake imepiga hatua kubwa katika ukusanyaji na utoaji wa takwimu bora na hivyo kuiwezesha kushika nafasi ya pili barani Afrika ikitanguliwa na Ofisi ya Takwimu ya Afrika Kusini.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu, Mabalozi, Mwakilishi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia Bi. Bella Bird na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Dkt. Binilith Mahenge.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
20 Desemba, 2017
SOURCE.IKULU
Maoni