KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU

KARAMA ZA UWEZO
i)             Karama ya Imani
Awali ya yote, kabla sijaichambua karama ya imani, hebu nitoe
tafsiri fupi ya msamiati wa neno imani kibiblia ina maana gani. Imani ni
“hisia ya rohoni za kuwa na hakika na mambo ya ki-Mungu zikiwemo ahadi
zake pamoja na kutambua uwepo wake kama Mungu Muumbaji na mwenye uwezo wote,asiyeshindwa lo lote na yuko mahali pote na anajua mambo yote.
Kitabu cha Waebrania kimeandika kwamba: “Basi, imani ni KUWA na
hakika ya mambo yatarajiwayo, na bayana ya mambo yasiyoonekana bado.” (EBR
11:1)
Imani hii chanzo chake ni Injili ya wokovu inapohubiriwa kwa
mwenye dhambi, akaisikia ndipo hushawishika na kuanza KUWA na hakika ya
ukombozi wa Yesu Kristo. Kitabu cha Warumi kimeandika chimbuko la Imani kuwa: “chanzo cha imani ni kusikia, na kusikia kunatokana na Neno la Kristo.”
(Rum.10:17)
Kila mwamini aliyeokoka anayo imani ya Kristo. Kwa imani hiyo,
amepokea wokovu na kuhesabiwa haki mbele za Mungu. Haya sasa tuje kwenye
tafsiri ya karama ya Imani kama ifuatavyo:
Karama ya Imani ni uwezo maalum wa Roho Mtakatifu unaoshukia au
kujazwa ndani ya mtu ambaye amejaliwa/kutumiwa na Roho kwa ajili ya kufanya
jambo/tendo kubwa ambalo liko nje ya uwezo wa kawaida wa kibinadamu. Karama
ya Imani ni uwezo maalum wa KUWA na hakika/ujasiri wa kuchukua hatua kufanya
jambo ambalo linahitaji uwezo kutoka kwa Mungu peke yake ndipo lifanikiwe
Karama ya imani humwezesha mhusika kukabiliana na changamoto au
upinzani mkali na akamudu kushinda wakati waamini wengine wamekata tamaa
kabisa. Karama ya imani ni moja ya karama za nguvu ambayo pia huzichochea
zile karama za kuponya magonjwa na matendo ya miujiza kutenda kazi zake. 
Na pia ili karama nyingine ziweze kufanya kazi lazima karama ya
Imani imwingie muhusika na kumpa uwezo wa kutumiwa kwenye maeneo mengine. Kwa mfano kitendo cha Yesu kutembea juu ya maji kilihusisha karama mbili mojawapo
ikiwa ni karama ya imani. 
Kitendo cha kufufua wafu kilihusisha karama mbili ikiwemo karama
ya Imani. Kitendo cha Yesu kubariki mikate michache wakala watu zaidi ya elfu
tano kilihusisha karama mbili mojawapo ikiwa ni karama ya Imani. Kwa hiyo
karama ya Imani ni kama ufunguo wa utendaji wa  fungu la karama za NGUVU.
Hapo awali nilisema kila mwamini Aliyezaliwa mara ya pili anayo
imani ambayo ndiyo ilimwezesha kupokea wokovu na baraka za kiroho. Kwa imani
hiyo mwamini anahesabiwa haki mbele za Mungu. Lakini si kila mwamini
ambaye anaweza kutumiwa na Karama ya Imani.
ii)            Karama za kuponya magonjwa
Kuna tofauti kubwa kati ya uponyaji na tiba. Tiba ni inahusiana
na matumizi ya dawa katika kutibu magonjwa. Uponyaji ni uwezo wa kuondoa
magonjwa au kurejesha afya njema pasipo matumizi ya dawa au lishe maalum.
Ni kutokana na aina hii ya uwezo wa kuondoa maradhi au magonjwa
katika mwili wa binadamu na akarejea kwenye afya njema, akawa mzima inaleta
msamiati wa kibiblia wa “Karama za kuponya magonjwa”!
Yesu Kristo ndiye mwanzilishi wa huduma za kuponya magonjwa na
akiwa ndiye Mponyaji Mkuu wa magonjwa yote. Aidha, ni Yesu ALIYETOA mamlaka kwa wanafunzi wake wanapotangaza Injili yake wafanye maombezi ya kuponya magonjwa.
Sasa tuje kwenye utendaji wa hii karama za kuponya magonjwa. Hii
inaitwa karama za kuponya magonjwa katika wingi badala ya umoja. Maana yake
karama za kuponya ziko zaidi ya karama moja. Hizi karama za kuponya
magonjwa ziko katika wingi kwa sababu na magonjwa yako ya aina nyingi pia. Kwa
mantiki hii kila aina ya ugonjwa ipo karama maalum ya kuushughulikia. 
Lakini pia karama za kuponya ziko katika wingi kwa maana kwamba,
Roho Mtakatifu huzigawa karama za kuponya kwa waamini tofauti tofauti badala ya
mwamini mmoja kutumiwa katika karama za kuponya magonjwa yote. Wako
waamini wanaotumiwa kuponya aina fulani ya magonjwa, au kuponya baadhi ya
magonjwa na sio magonjwa yote.
 Huu ni mgawanyo wa Roho Mtakatifu akitaka kuwatumia
waamini tofauti ili kudhibiti mtu mmoja kuhodhi kila karama kwa magonjwa yote.
iii)            Karama ya matendo ya miujiza
Karama ya matendo ya miujiza maana yake ni uwezo wa kiungu wa
kufanya mambo ambayo yako katika uwezo wa asili wa kibinadamu. Kwenye karama ya
miujiza kama jina lake lilivyo kazi yake kufanya mambo ya kushangaza na kutisha
yaliyoko nje ya uwezo wa kanuni za asili. Maana ndani ya karama ya miujiza
ndimo ulimo uwezo wa uumbaji wa kimungu. Mathalan, Yesu kutungwa mimba kwa
uwezo wa Roho Mtakatifu ni karama ya matendo ya miujiza.
Huko nyuma nimeeleza kwamba karama ya kutenda miujiza hufanya
kazi bega kwa bega na “karama ya Imani” maana zinategemeana sana, tofauti na
karama za kuponya magonjwa. Karama ya matendo ya miujiza inahusisha matendo
yote kuanzia kurejesha upya viungo vya mwili vilivyoharibika mpaka uwezeshaji
wa vitu chache kutosheleza mahitaji makubwa kuliko uwezo wake wa kawaida.
Kwa kupitia karama ya miujiza, Roho Mtakatifu ndani ya mwamini
anaweza kumtumia kufanya jambo ambalo ni la kushangaza na waisoamini
wakamtukuza Mungu kwa ajili ya tukio hilo.
Naomba kutoa tahadhari hapa kwamba, kuna vituko vingi siku hizi
katika huduma za kimaombezi ambavyo vinaitwa miujiza lakini sio utendaji wa
“karama ya miujiza”. Mfano vitendo vya watu kuanguka chini kwa mkupuo vinatafsiriwa
kuwa ni “karama ya miujiza” wakati ukweli sio.
Ni kweli kwamba Inashangaza kwa macho! Shetani naye anaweza
kuangusha watu saaana tu. Sasa kitu ambacho Ibilisi anaweza kukitumia kwa
urahisi kudanganya watu kama kiini macho au mazingaombwe hakiwezi kutafsiri
kuwa hiyo ni karama ya miujiza inayotendwa na Roho Mtakatifu.
Karama ya miujiza hutenda jambo ambalo Ibilisi hawezi kuigiza au
kulifanya kwenye mazingira ambayo Roho Mtakatifu anatawala.
Kwa mfano watumishi wa Ibilisi nao wanaweza wakacheza na mapepo
kwenye mikutano ya hadhara, lakini sio kwamba huwa wanatoa pepo. Wao “wanapunga
pepo” badala ya “kutoa pepo”. Lakini matukio yote yanahusisha udhuhuriko wa
mapepo. Hapa ndipo inahitaji ile “Karama ya kupambanua roho” ili kutofautisha
muujiza wa Roho Mtakatifu na mazingaombwe na viini macho vya Ibilisi.











Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

KUFANIKIWA KI -UCHUMI KWA NJIA YA MUNGU

UCHAMBUZI WA KITABU CHA DANIELI

SOMO: NGUVU YA DAMU YA YESU KATIKA KUWEKA AGANO