NAFASI YAKO NI MUHIMU SANA KATIKA KUUJENGA MWILI WA KRISTO
Na: Patrick Sanga
Biblia katika 1 Wakorinto 12:11-14,18
imeandikwa ‘Lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule,
AKIMGAWIA kila mtu peke yake kama apendavyo yeye. Maana kama vile mwili ni mmoja,
nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili
mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa
kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa
au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja. Kwa maana mwili si kiungo
kimoja, bali ni VINGI. Bali Mungu AMEVITIA viungo kila kimoja katika
mwili kama ALIVYOTAKA’ (1Wakorintho 12:1-31, Warumi 12:4-8)
Kanisa ni mwili wa Kristo wenye viungo
vingi, naam, kila kiungo kinao wajibu (unique) wa kufanya ili kuujenga mwili
wa Kristo na kuusaidia kufikia malengo yake ipasavyo. Naam ili kutekeleza
wajibu huo, kila kiungo kimepewa uwezo na kimewekewa namna (mipaka) yake ya
utendaji kazi ambayo matokeo yake yanaathari kwa mwili mzima. Kumbuka
mwenye kugawa wajibu kwa kila kiungo ikiwa ni karama, vipawa au huduma sambamba
utendaji kazi wake ni Mungu.
Hii ina maana sisi kama viungo katika
mwili wa Kristo, kila mmoja anamuhitaji mwenzake maana anacho kitu cha
kuufaa mwili mzima. Wapo watu ambao katika ulimwengu wa roho ni mikono,
moyo, ubongo, mapafu, midomo, macho (wanaona tusivyoona), masikio,
miguu, pua, maziwa, viungo vya uzazi, viungo vya kutoa uchafu nk. Jambo muhimu
ni kwamba, kila mmoja lazima afanye wajibu wake huku akishirikiana, kutia moyo
na kuombea viungo vingine kila kimoja kifanye kazi yake pia, ipasavyo.
Ndio maana katika 1Wakorinto
12:17,21-24 imeandikwa ‘Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? Kama
wote ni sikio ku wapi kunusa? Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na
wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi. Bali
zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa
zaidi. Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile
twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana.
Kwa maana viungo vyetu vilivyo na uzuri HAVINA UHITAJI; bali Mungu
ameuungamanisha mwili, na kukipa heshima zaidi kile kiungo kilichopungukiwa’.
Watu (viungo) wanaoonekana kuwa
wanyonge, wadhaifu, hawana heshima au wana upungufu, katika ulimwengu wa
roho wamepewa uwezo mkubwa zaidi katika utendaji wa mwili wa Kristo. ikiwa
sisi tunaona havina uzuri, tambua uzuri wao ni ule usioonekana kwa macho ya
damu na nyama, bali macho ya kiroho pekee.
Rejea mstari wa 24 ‘viungo vizuri
havina uhitaji’, kwa sababu havioni haja ya kumtafuta Mungu kwani vinaamini
vinajitosheleza au vimekamilika. Fikra hii ndiyo inayovifanya viungo hivi
kudharau au kutotambua umuhimu (nafasi) wa viungo vingine katika utendaji wa
mwili wa Kristo. Naam, Mungu kwa kulijua hilo akaweka utaratibu wa kujifunua
kupitia udhaifu au upungufu wa mtu. Naam hii ni kwa sababu uweza wa Mungu
unatimilika katika madhaifu, umefichwa na unakaa juu ya vinavyoonekana kuwa
vinyonge, vidhaifu (2Wakorntho 12:7-10).
Kutokana na upungufu au unyonge wao
wanapokea mafunuo zaidi na hii ni kwa sababu ya utaratibu wa Mungu kujidhirisha
(kujifunua) kupitia mdahaifu au mapungufu ya mtu. Madhaifu, masumbufu, adha au
shida walizonazo zinawafanya wawe karibu zaidi na Mungu. Na kwa kwa sababu
Mungu haonekana kwao wamtafutao, anapowajibu si tu atasema kwa ajili yao pekee
bali zaidi kwa ajili ya mwili wa Kristo.
Usidharau wengine kwa kuwa huwezi kujua
nani anahusika moja kwa moja na maisha yako ya kila siku. Naam anaweza kuwa
yule ambaye kwa jinsi ya kibinadamu haumpi heshima au umuhimu unaostahili, au
unaona hana msaada kwako. Hawa ni watu ambao wanashughulika na maisha yako bila
wewe kujua (viungo vya ndani, undercover agents). Naam wameitwa hivyo na
wamepewa maelekezo ya aina hiyo na Mungu wao, jambo muhimu wewe waombee na si
kuwasema vibaya.
Kumbuka kwamba kanisa lolote linaundwa
na familia, hivyo sharti dhana hii ya kutambua nafasi ya mtu mwingine lianzie
kwenye ngazi ya familia, ndoa zetu pia. Ukitambua nafasi ya mweza wako, walezi
au watoto wako utawapa umuhimu waostahili kwani ndio viungo vya mwili wa
Kristo. Kuna watu wanashindwa kumtumikia Mungu ipasavyo kwa sababu ya
changamoto ya ndoa zao (Waefeso 5:22-27 vs 1Wakorintho 7:25-28)
Je unaitumiaje nafasi na uwepo wako
katika kuujenga mwili wa Kristo? – Biblia katika Mtahayo 24:45-46 inasema ‘Ni
nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya
nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana
wake ajapo atamkuta akifanya hivyo’.
Ukienda kwenye Luka 12:47-48 imeandikwa
‘Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala
kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana. Na yule asiyejua, naye amefanya
yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo
vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na
zaidi’ (Rejea Luka 12:42-48).
Mambo muhimu kuzingtia kama kiungo cha
mwili wa Kristo:
- Uwe mwaminifu kwenye eneo la wito wako kama kiungo katika mwili wa Kristo. Dumu kuwaombea na kuwatia moyo watu (viungo) wengine kwa sababu kadri wanavyofanya wajibu wao pia ipasavyo, ndivyo na mwili wa Kristo unavyoongezeka. Usiwe chanzo cha mwili kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo au kukwamisha viungo vingine vishindwe kufanya kazi kwa maneno au matendo yako. Ikiwa hujui wajibu wako ni nini, uliza kwa Mungu ili uwe na uhakika kitu gani umepewa kufanya katika mwili wake, kutokujua sio uetetezi, utahukumiwa kwa kutokujua kwako?
- Fanya sehemu yako, usione wivu wala usijaribu kujilinganisha na mtu au watu wengine kwa sababu kila mmoja ameitwa na kupewa uwezo (vipawa) kama Mungu apendavyo. Naam tumeitwa tofauti wapo waliopewa vingi, wapo waliopewa kidogo, na kila mmoja atawajibika kwa nafasi yake.
- Usiruhusu mapito, maneno ya watu au changamoto unazopitia zikuzuie kutekeleza wajibu wako kwa sababu mbele zake Bwana huo sio utetezi. Tena wala usiruhusu Shetani kupitia uongo (roho zidanganyazo) wake akuondoe kwenye kuyatenda mapenzi ya Mungu. Kumbuka vipo viungo vionekanavyo na visivyonekana.
- Ongeza na kudumisha upendo wako kwa wengine, maana, upendo haupungui neno wakati wowote. Kumbuka imeandikwa ‘Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo’ (1Wakorinto 13:1-2,13)
Hitimisho: Tambua kwamba haupo
ulipo kwa bahati mbaya, bali umewekwa hapo kama kiungo muhimu katika
uendeshaji na utendaji wa mwili wa Kristo. Kila mmoja amepewa (entrusted)
wajibu wa kufanya katika kuujenga mwili wa Kristo. Pale unapolala
(kutowajibika) unaugharimu mwili wote kwa kutoa nafasi ambayo Shetani anaitumia
kuleta athari kwa mwili mzima. Usisahau kwamba muda wa kutoa hesabu kwa Bwana
aliyekupa wajibu huo unakuja (Mathayo 25:14-29).
Utukufu na Heshima vina wewe Yesu,
wastahili BWANA
Maoni