WOKOVU NI KUWA NA USHIRIKA
SEHEMU YA KWANZA
KWELI KUU:
Maisha
yetu ya wokovu hayana maana kabisa kama hatutakuwa na ushirika na Baba,
Mwana, Roho Mtakatifu, na sisi kwa sisi kama kanisa la Kristo ambalo ni
mwili wa Kristo.
Mstari wa Msingi (Kukumbuka):
1 Wakorintho 1:9
Mungu ni mwamainifu ambaye mliitwa na yeye mwingie katika ushirika wa Mwanawe, Yesu Kristo Bwana wetu.
Ndugu mpendwa, leo nitaanza mfululizo wa somo hili ambalo litakuwezesha wewe kueneza mizizi yako ya imani katika Yesu Kristo Bwana wetu ambaye ni Mungu Mwana, na katika Mungu Roho Mtakatifu na katika Mungu Baba kwa kujua nini maana ya kuwa na ushirika, namna ya kuwa na ushirikana jinsi ya kuendelea kuwa na ushirika Mungu (Baba, Mwana na Roho Matakatifu). Karibu sana.
UTANGULIZI:
Katika utangulizi wetu, tutaangalia zaidi maana ya maneno makuu matatu ambayo yatajitokeza katika somo letu hili na miongoni mwa maneno hayo mawili yamejitokeza katika kichwa cha somo letu. Hivyo ni lazima tuyaangalie ili tuwe na nafasi nzuri ya kuelewa somo letu; maneno hayo ni pamoja na wokovu, ushirika na uhusiano au mahusiano.
USHIRIKA NI NINI?
Ushirika ni hali ya kuwa pamoja kwa umoja, kushirikiana na kuwa kitu kimoja katika mambo yote yaliyowaweka watu pamoja. Ushirika ni kuambatana kwa kuwa kitu kimoja na kuwa na shirika katika mambo yote yaliyowaweka watu pamoja.
Haiwezekani kuwa na ushirika pasipo kuwa na mahusiano au uhusiano wowote. Ushirika ni matokeo ya kuwa na mahusiano baina ya watu wawili au pande mbili za watu. Ijapokuwa haiwezekani kuwa na ushirika pasipo kuwa na mahusiano, lakini kwa upande mwingine inawezekana kabisa kuwa na mahusiano lakini kusiwepo na ushirika. Na ili mahusiano yoyote yawe imara na yenye matunda kwa wahusiaka ni lazima yaambatane na ushirika kwa wawili hao kuwa na ushirika binafsi kila mmoja kwa mwenzake.
Pengine unaweza ukawa bado hujanielewa na hujaweza kutofautisha kati ya ushirika na mahusiano; usiwe na shaka, utanielewa tu kwa kadiri tutakavyokuwa tunaendelea na somo hili. Kabla sijaendelea sana, tuangalie kwanza mahusiano ni nini.
MAHUSIANO NI NINI?
Mahusiano ni hali ya muunganiko (a connection) kati ya watu wawili (au pande mbili za watu; kati ya mtu na mtu, watu na mtu au mtu na watu) unaowafanya wahusiane moja kwa moja (direct) au kupitia mtu mwingine (indirect). Mahusiano ni kuhusiana kwa namna yeyote ile, na mfano wa mahusiano ni pamoja na;
- Baba na mwana (huu ni uhusiano wa mtoto na mzazi wake wenye muunganiko kwa njia ya kuzaa na kuzaliwa, muunganiko wa damu),
- Mume na mke (huu ni uhusiano wa kindoa, ni uhusiano wenye muunganiko wa kiagano; agano la ndoa),
- Mwalimu na mwanafunzi,
- Mchungaji na kondoo,
- Kaka na dada (huu ni uhusiano wa ndugu wenye muunganiko wa
kuzaliwa pamoja aidha kwa kuchangia wazazi wote wawili au mzazi wa pande
moja (baba au mama),
- Mfanyakazi na mfanyakazi; mfanyakazi na bosi wake,
- Mwamini na mwamini,
- Mungu (Baba) na mwanadamu (mtoto au mwana wake) na kadhalika
Hiyo juu ni mifanao ya mahusiano, na mahusiano yote haya yanaweza yakawepo lakini pamoja na uwepo wa mahusiano haya inawezekana kabisa usiwepo ushirika baina ya wahusika waliopo katika mahusiano hayo. Na ili mahusiano yawe na maana (yafikie malengo yake, na yazae matunda) ni lazima yagubikwe (characterized) na ushirika baina ya hawa watu wawili wenye uhusiano.
VIINI (ESSENCES) VYA USHIRIKA
UMOJA
Kiini (essence) kimojawapo cha ushirika katika mahusiano ni umoja (oneness) katika mambo yote walionao wahusika wa mahusiano hayo, iwe mke na mume, baba na mtoto, kaka na dada n.k; nia moja, mapenzi mamoja, kusudi moja n.k.
UPENDO
Kiini (essence) kingine cha ushirika ni upendo walionao wahusika kila mmoja kwa mwenzake; huwezi kuwa na ushirika mahali ambapo upendo haupo, mahusiano yoyote ambayo wahusika wake wamepungukiwa na upendo au upande mmoja au pande mbili zote huwa yamekosa ushirika; ushirika ndio unaowafanya wawili wawe mmoja katika yote yaliyowaweka pamoja na katika mahusiano yao. Kwa hiyo, upendo unapokosekana, ushirika hutoweka kabisa.
MUDA
Kiini (essence) kingine cha ushirika ni muda wa kuwa pamoja kwa ajili ya mwenzako na kufanya mambo yote kwa pamoja. Ushirika unahitaji muda wa kuwa pamoja wa wawili ambao wapo kwenye mahusiano yoyote ili waweze kushirikiana katika mambo yao; kila mmoja ashiriki mambo ya mwenzake na kila mmoja amshirikishe mwenzake mambo yake kwa kuwa na mazungumzo, na hatimaye wote wawili wawe na wakati mzuri wa kufanya mambo yote kwa pamoja.
UHUSIANO NA USHIRIKA
Yohana 10:30, 37, 38
[30] Mimi na Baba tu umoja.
[37] Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini;
[38] lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziamini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba.
[37] Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini;
[38] lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziamini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba.
Katika kifungu cha maandiko hapo juu, anaposema, “Mimi na Baba” hapo anaanza kwa kutambulisha uhusiano kati yake na Baba, Yesu akiwa Mwana wa Baba (ambaye ndiye Mungu Baba); huu ni uhusiano wa Baba na Mwana.
Lakini anaposema kuwa “tu umoja” hapo anatambulisha ushirika walionao wawili hao ambao unamfanya Yesu atende kazi za Baba yake (msitari 37); na katika msitari wa 38 anafafanua ushirika huo ni kwa namna gani upo kati yao wawili hao; ndipo anasema kuwa, Baba yu ndani yake na Yeye yu ndani ya Baba.
Ili upate kunielewa hapa, anaposema Baba yu ndani yake na Yeye ndani ya Baba, sina budi kutumia mfano huu; Ukichukua sharubati (juice) ya embe na sharubati ya nanasi ukavichanganya kwa pamoja katika chombo kimoja, na kisha ukatikisa, sharubati ya embe itakuwa ndani ya sharubati ya nanansi na sharubati ya nanansi itakuwa ndnai ya sharubati ya embe. Vyote viwili vitakuwa kitu kimoja, na radha utakayoisikia katika sharubati hiyo (ya embe na nanasi) itakuwa ni radha ya pamoja, na kamwe huwezi kurudi na kuzitenganisha sharubati ya embe ikae peke yake na ya nanasi ikae peke yake. Tayari hivi viwili vimekuwa na shirika; ndivyo alivyo Yesu Mwana na Baba Mungu.
Yohana 15:5
Mimi
ni mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo
huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamuwezi kufanya neno lolote.
“Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi”, hapa Yesu anatambulisha uhusiano wake na wanafunzi wake waliomwamini (kanisa lake), Yeye akiwa ni mzabibu, na wanafunzi wake wakiwa ni matawi ya mzazibu; huu ni uhusiano.
“Akaaye ndani yangu nami ndani yake” huu ni ushirika kati ya Yesu na wanafunzi wake. Kuwa na ushirika ni kukaa ndani ya Yesu na Yesu kukaa ndani yako; huku ni kuwa umoja (oneness) baina ya wawili wenye mahusiano.
“Huyo huzaa sana”, haya ni matokeo ya kuwa na ushirika baina ya watu walio na mahusiano au uhusiano. Hebu fikiria, binti na kijana wameoana lakini wakakaa tu wasishiriki tendo la ndoa (wasiwe na ushirika wa tendo la ndoa), watazaaje? Kamwe hawataweza kuzaa watoto hata kama watakaa miaka 1000 maadamu tu hawatashiriki tendo la ndoa.
Ushirika wowote huwa na matunda pindi wahusiaka wanapodumu katika kuwa na ushirika huo. Usisahau kuwa, somo letu ni Wokovu Ni Kuwa Na Ushirika; na sasa tunaangalia utangulizi wa somo letu hili ambao utatusaidia kuelewa kiini cha somo.
Katika sehemu ya pili ya somo letu, tutakuwa tunaangalia Wokovu ni nini. Mungu akubariki sana na kukusaidia kwa Roho wake Mtakatifu kuyaelewa haya ili iwe ni kwa afya ya roho yako na uzima wako.
Na,
Mch. Ezekiel P. Bundala
0673 184 468
Maoni