KWELI KUU:
Maisha
yetu ya wokovu hayana maana kabisa kama hatutakuwa na ushirika na Baba,
na Mwana, na Roho Mtakatifu, na sisi kwa sisi kama kanisa la Kristo
ambalo ni mwili wa Kristo.
Mstari wa Msingi (Kukumbuka):
1 Wakorintho 1:9
Mungu ni mwamainifu ambaye mliitwa na yeye mwingie katika ushirika wa Mwanawe, Yesu Kristo Bwana wetu.
UTANGULIZI
Katika utangulizi, sehemu ya kwanza ya somo letu tuliangalia maana ya “ushirika” na maana ya “uhusiano au mahusiano”
na pia tulipata kubainisha na kuainisha kwa kifupi sana viini
(essences) vya ushirika. Leo katika utangulizi wetu nataka twende mbele
kidogo kwa kuangalia ni nini maana ya “wokovu”; usisahau somo letu ni “Wokovu Ni Kuwa Na Ushirika” na bado tupo kwenye utangulizi ambapo tunaangalia maana ya maneno muhimu; wokovu, uhusiano na ushirika.
WOKOVU MAANA YAKE NINI?
Wokovu ni ukombozi wa mwanadamu kutoka katika vifungo vyote vya mauti na kuzimu kwa kusamehewa dhambi ili kuingizwa katika uzima wa milele.
Kuokoka ni kukombolewa kutoka katika vifungo vya mauti na kuzimu kwa
kusamehewa dhambi na kutakaswa kwa damu ya Yesu Kristo na kuingizwa
katika uzima wa milele; na wokovu huu unapatikana kwa njia ya kumwamini
Yesu Kristo ambapo mtu huamini moyoni mwake na kwa kinywa chake hukiri
ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, aliteswa, alikufa, akazikwa na siku ya
tatu Mungu alimfufua kutoka katika wafu, na ya kuwa aweza kutuokoa na
maasi yetu yote na kuzimu na mauti.
Tendo hili ni tendo linalotuingiza katika ushirika na Mungu kwa kuwa na mahusiano naye ya Baba na wana, kwa maana wote waliompokea Yesu Kristo walipewa uwezo wa kufanyika wana (watoto) wa Mungu kwa kuliamini Jina la Yesu Kristo.
Wokovu ni kufunguliwa kutoka katika vifungo vyote vya maovu na mabaya
yote na kutoka katika utumwa wa dhambi ili kuwekwa huru kisha kuingizwa
katika raha ya milele.
Wokovu ni kuhifadhiwa kutoka katika (au mbali na) hatari, au madhara
yote yatokanayo na dhambi zetu tulizotenda; ni kuepushwa na hukumu ili
kuhifadhiwa salama milele yote.
Kwa hiyo, wokovu ni kukombolewa, kufunguliwa na kuhifadhiwa; ukiokoka
wewe unakuwa umekombolewa, umefunguliwa na umehifadhiwa kutoka katika
ufalme wa giza na mambo yake yote.
Wakolosai 1:13 – 14
[13] Naye alituokoa (kutoka) katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;
[14] ambaye katika Yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;
Wokovu umejumuisha mambo matatu ambayo yanafanyika kwa wakati mmoja;
kutolewa katika nguvu za giza, kuhamishwa kutoka huko, na kisha
kuingizwa katika ufalme wa Yesu Kristo ambapo ndani yake tunao ukombozi,
yaani kusamehewa dhambi zetu zote na kuondolewa kwa madhara yote
yatokanayo na dhambi.
Mtu anapompokea Yesu maishani mwake papo hapo anatolewa (au anaondolewa)
katika nguvu za giza, anahamishwa kutoka huko, na kisha anaingizwa
katika ufalme wa Yesu Kristo; na hapa ndipo maandiko husema, “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Yesu Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! yamekuwa mapya” 2Wakorintho 5:17.
Mtu anapopokea wokovu au anapokuwa ameokoka anakuwa amekombolewa,
amefunguliwa na amehifadhiwa kwa kutolewa kutoka katika nguvu za giza,
kuhamishwa kutoka huko, na kuingizwa katika ufalme wa Yesu Kristo Bwana
wetu.
Hakuna wokovu bila kutolewa, kuhamishwa na kuingizwa; “Bwana akaonya
ishara na maajabu, makubwa, mazito, juu ya Misri, na juu ya Farao, na
juu ya nyumba yake yote, mbele ya macho yetu; akatutoa huko ili
kutuingiza huku, apate kutupa nchi aliyowaapia baba zetu.” Kumbukumbu 6:22 – 23.
Wokovu ni kutolewa huko (katika ufalme wa giza kupitia kazi ya msalaba)
na kuingizwa huku (katika ufalme wa nuru; ufalme wa Yesu Kristo) ili
tupate yote tuliyokirimiwa na Mungu tangu kuumbwa misingi ya ulimwengu.
Hii maana yake ni kwamba, huwezi kupewa uzima wa milele na yote ambayo
umekirimiwa na kuahidiwa na Mungu kama utakuwa hujaokoka (hujatolewa
huko na kuingizwa huku); na huwezi kuingizwa huku kabla hujatolewa huko.
Kutoka 6:6 - 7
[6] Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni YEHOVA, nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya mizigo ya Wamisri, nami nitawaokoa na utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa,
[7] nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, Mungu wenu, niwatoaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri.
[8] Nami nitawaleta hata nchi hata nchi ile ambayo naliinua mkono wangu niwape Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, nitawapa iwe urithi wenu; Mimi ni Yehova.
Ninachotaka wewe ukione katika maandiko haya ni maana halisi ya wokovu;
haiishii tu kutolewa, kuhamishwa, na kuingizwa bali pia kupewa;
unatolewa katika nguvu za giza, unahamishwa kutoka huko, unaingizwa
katika ufalme wa Yesu Kristo na unapewa ufalme huo kuwa urithi wako; na
hapa ndipo Biblia inaposema ya kuwa, “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye” Warumi 8:16, 17.
Kama sisi tu warithi pamoja na Kristo, alichopewa Yesu ndicho
tulichopewa sisi, na Yesu amepewa ufalme, hii maana yake na sisi
tumepewa ufalme kwa kuwa ndani ya Yesu Kristo; tunapoingizwa pia
tunapewa; vyote vilivyo vya Yesu vinakuwa vya kwetu, na hii ni kwa njia
ya kuwa na ushirika naye usiokuwa na mwisho. Kwa hiyo, wokovu
haukamiliki pasipo wewe kupewa huo ufalme ambao wewe umeingizwa ndani
yake. Unapopewa ufalme huo, ufalme huo unakuwa ndani yako wewe (Luka 17:21; “....kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu”).
Kilicho ndani yako ni kile tu ulichopewa na Mungu; na wewe kwa kumpokea
Yesu Kristo umepewa ufalme na vyote vilivyomo ndani ya ufalme huo.
Mathayo 16:19
Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.
Aliyepewa ufunguo wa ufalme ndiye aliyepewa ufalme; tunapookolewa na
kuwa wa Mungu, tunapewa funguo za ufalme, hii maana yake tunakuwa
tumepewa ufalme wenyewe. Ufunguo ni mamlaka; kama tumepewa mamlaka ya
ufalme ili kufungua na kufunga, hii maana yake tumepewa ufalme wenyewe,
na huu ndio wokovu; tunatolewa, tunahamishwa, tunaingizwa, na kisha
tunapewa ili tuwe na nguvu dhidi ya ufalme wa giza.
Katika msitari wa 7 anasema, “Nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa Mungu kwenu”,
hapa anazungumzia uhusiano na ushirika atakaouanzisha na watu wale
atakaowaokoa. Haiwezekani kuwepo kwa wokovu pasipokuwepo na ushirika, na
ndio sababu nataka tujifunze kweli hii ili kuimarisha uhusiano wetu na
Mungu kwa kuwa na ushirika naye pamoja na watu wake.
Mtu anakuwa ameokoka pale tu anapokuwa ndani ya Yesu Kristo; hapa
anakuwa ametolewa katika nguvu za giza; yaani amefunguliwa kutoka katika
vifungo vyote vilivyomfunga, amehamishwa kutoka huko; yaani ameondolewa
kabisa ndani ya ufalme huo wa giza, ameingizwa katika ufalme wa Mwana
wa pendo lake; yaani yumo ndani ya Yesu Kristo, na amepewa ufalme
(amerithishwa ufalme pamoja na Yesu Kristo), amepewa funguo za ufalme,
sio tena mtumwa na mfungwa, bali ni mtawala anayetawala pamoja na Yesu
Kristo kwa sababu anao ukombozi kwa kuwa amesamehewa dhambi zake zote.
Napenda wewe uelewe jambo hili, kule kusema kwamba, “Kuwa ndani ya Yesu” huko ndiko kunaitwa kuwa na ushirika;
aliye ndani ya Yesu Kristo ana ushirika na Baba, na Mwana, na Roho
Mtakatifu, kwa sababu wote hawa huja na kufanya mako ndani ya mtu huyu.
Lakini pia aliye ndani ya Yesu Kristo yupo ndani ya kanisa kwa sababu
yeye mwenyewe ni kanisa, na kwa maana hiyo atakuwa na ushirika pia na
kanisa la Mungu kwa maana ya jumuiya ya watu waliomwamini Yesu Kristo,
wale waliookolewa na kukombolewa kwa damu ya Yesu Kristo. Sasa kudumu
katika ushirika na Baba, na Mwana, na Roho, na Kanisa ndio wokovu
wenyewe.
Mtu mwenye ushirika na Baba ni mmoja naye, anampenda Baba, na ana muda
naye, vivyo hivyo kwa Mwana na kwa Roho Mtakatifu lakini pia na kwa
Kanisa. Ukweli ni kwamba, ambaye una ushirika naye, utakuwa umoja naye,
utampenda, na utampa muda wako bora kabisa na wa kutosha na si bora muda
ili upate kumfanyia mambo na yeye kukufanyia mambo na ili muwe na
mazungumzo ya pamoja na kushiriki vitu vyote pamoja.
Mpendwa kuokolewa ni kuitwa ili uingie kwenye ushirika na Yesu Kristo;
na kwa kuwa na ushirika na Yesu Kristo, unakuwa na ushirika na Mungu
Baba, na Roho Mtakatifu, na kanisa; kuanzia hapa sasa nataka kipengele
kwa kipengele, hatua kwa hatua tuangalie huko kuwa na ushirika na Baba,
na Mwana, na Roho Mtakatifu, na Kanisa ni kwa namna gani. Usikose sehemu
ya tatu ya somo letu ambapo tutaanza kiini cha somo.
Mungu akubariki sana.
Na,
Mch. Ezekiel P. Bundala
0673 184 468
0752 184 464
Maoni