NAMNA MWANAMKE ANAVYOWEZA KUTUMIA NAFASI ZAKE KUBADILISHA MAISHA YA NDOA YAKE (Sehemu ya 3)
Na: Patrick Sanga
Nafasi ya nne – Mwanamke kama Mlinzi
Katika sehemu ya pili tuliangalia nafasi tatu za awali ambazo ni nafasi ya Msaidizi, Mshauri na Mleta kibali. Ili kusoma sehemu ya pili bonyeza link hii https://nsanacz.blogspot.com/2018/05/namna-mwanamke-anavyoweza-kutumia_4.html .Kumbuka
kwamba lengo la ujumbe ni kuangalia ni kwa namna gani Mwanamke
aliyeolewa anaweza kutumia nafasi zake kubadilisha/kuiponya ndoa yake.
Katika sehemu hii ya tatu tutaangalia nafasi ya mwanamke kama Mlinzi.
Naam kwa rejea kumbuka kwamba, msingi wa somo hili ni maneno ambayo
Octoba 2009 BWANA aliniambia akisema ‘Waambie wanawake wasimame kwenye nafasi zao ndipo wataona uponyaji kwenye ndoa zao’.
Labda nianze kwa kuuliza, je una fahamu kwamba wajibu wa kumlinda mumeo ni wako? Naam Mungu amejiwekea utaratibu mpya kwamba Mwanamke amlinde mwanaume.
Je ni ulinzi wa namna gani? Ni ulinzi wa kiroho ndio ambao mwanaume
anahitaji kutoka kwa mkewe. Mke anatakiwa kuwa makini ‘sensitive’ katika
ulimwengu wa roho kuangalia ni mashambulizi gani Shetani amekusudia
kuyaleta kwa mume/ndoa yake. Naam akishajua aweke ulinzi ili mawazo ya
Shetani yasitimie kwenye ndoa yake.
Kuwa Mke wa fulani, ni nafasi ya
ulinzi katika ulimwengu wa roho ambayo Mungu anaitoa. Kwa hiyo fahamu
kwamba unapoingia kwenye ndoa, Mungu anakupa wajibu wa kumlinda mumeo.
Biblia katika Yeremia 31:22 inasema ‘Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana BWANA ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanaume.
Nafasi ya ulinzi ni nafasi ya pekee sana ambayo Mwanamke amepewa na
endapo ataitumia vizuri itamsaidia kweli kweli kuiponya ndoa yake. Hii
ni kwa sababu mlinzi ndiye anayeona mambo yanayotaka kuja kwenye ndoa
yake akali kwenye ulimwengu wa roho, kabla hayajadhihirika kwenye
ulimwengu wa mwili.
Ukisoma Mstari huu wa Yeremia 31:22 katika toleo la kiingereza la ESV unasema ‘How long will you waver, O faithless daughter? For the LORD has created a new thing on the earth: a woman encircles a man’ na pia katika toleo la KJV imeandikwa ‘How
long wilt thou go about, O thou backsliding daughter? for the LORD hath
created a new thing in the earth, A woman shall compass a man’.
Maneno ‘Mwanamke atamlinda mumewe’ kwenye ESV imeandikwa ‘a woman
encircles a man’ na kwenye KJV imeandikwa ‘A woman shall compass a man’.
Maneno haya yana maana ya zingira, zunguka au fanya duara.
Hapa Biblia inajaribu kutueleza jambo la
mwanamke ambaye yamkini kutokana na changamoto za ndoa yake/mume wake
alijikuta amekuwa mtu wa kuasi/kufanya mabaya. Sasa ili kumsaidia ndipo
BWANA akamtuma Yeremia kumweleza ‘acha kutanga tanga, Mungu ameumba
jambo jipya nalo ni ‘wewe mwanamke, umepewa wajibu wa kumlinda/kumzingira mwanaume/mumeo’.
Naam ulinzi huu ni kwa jinsi ya rohoni. Mwanamke anaweza
kumwekea/kumfanyia mume wake ulinzi dhidi ya makahaba, malaya, wenye
hila, wala rushwa au chochote ambacho ni chanzo cha uharibifu wa ndoa
nk.
Katika nafasi hii ya ulinzi Mke una wajibu wa kujua kwa nini Mungu amekuunganisha na mume uliye naye sasa.
Naam lipo kusudi la ufalme wake, hivyo ni jukumu lako kuhakikisha
linatimia katika siku zenu za kuwepo hapa duniani kama wanandoa. Naam
msaidie Mume wako kama Mlinzi kwa namna ambayo kusudi la Mungu
halitakwama kwenye maisha yenu. Fahamu kazi ya Mlinzi ni kumsaidia Bwana
wake kufanikisha majukumu yake. Endapo Mlinzi hatakuwa makini kwenye
nafasi yake basi majukumu ya Bwana wake hayatafanikiwa, si kwa sababu
ametaka bali ni kwa sababu Mlinzi/Walinzi wake hawakumpa usaidizi wa
kutosha kiulinzi.
Ni vizuri ukafahamu kwamba ili Shetani
ammalize mumeo, njia kuu kwake ni kupitia kwa mkewe. Angalia leo ndoa
ngapi zimeharibika na ukifuatilia chanzo utagundua Mke amechangia kwa
sehemu kubwa. Hebu taunaglie mifano kadhaa ndani ya Biblia;
Ndoa ya Anania na Safira (Matendo ya Mitume 5:1-11).
Ule msitari wa 1-2 maandiko yanasema ‘Lakini
Mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali,
akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta
fungu moja akaliweka miguuni pa mitume’. Ukisoma fungu zima hapo
juu utagundua kwamba kutokana na wizi wao wote wawili, walikufa siku
moja. Jambo ninalotaka tulione hapa ni ile kusema ‘mkewe naye akijua haya’.
Maneno haya yameandikwa ili kuonyesha namna ambavyo Safira hakutumia
nafasi yake kuiponya ndoa yake. Kutokana na kutokumshauri mumewe vizuri
na kumlinda dhidi ya hatari iliyokuwa mbele yao, wote wawili walikufa. Nani
ajuae kwamba pengine Safira angemwonya mumewe, mumewe angemsikiliza.
Naam kwa kuwa alinyamaza, na Mungu alinyamaza, mauti ikawajia.
Ndoa Ahabu na Yezebeli (1Wafalme 21:1-23)
Ukisoma andiko hili utaona namna
Yezebeli mke wa Ahabu alivyotumia vibaya nafasi zake, kwa kumuua Nabothi
ili amrithishe mumewe shamba la Nabothi. Biblia katika mstari wa 9 -10
inasema Yezebeli ‘ Akaandika katika zile nyaraka, akasema, pigeni
mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu, mkainue watu
wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki na kumshuhudia, kunena, umemtukana
Mungu na mfalme, kisha mchukueni nje mkampige kwa mawe, ili afe’.
Watu wa mji walifanya kama Yezebeli alivyoagiza. Naam Yezebeli hakujua
huo ndio ulikuwa mwisho wa utawala wao kwa kosa lile, kwani mahali pale
ambapo mbwa waliramba damu ya Nabothi ndipo na damu ya Ahabu
ilipomwagika wakairamba pia. Naam angekuwa na ufahamu huu, angetumia
nafasi zake vizuri kuponya ndoa yake na utawala wao juu ya nchi.
Ndoa ya Abramu na Sarai (Mwanzo 16:1- 6) nk.
Kutokana na Sarai kutokupata mtoto kwa
miaka mingi alimshauri Abramu mumewe atembee na mjakazi wake aliyeitwa
Hajiri pengine angepata mtoto. Maandiko yanasema Abramu akaingia kwa
Hajiri naye akashika mimba. Kitendo cha Hajiri kushika mimba kikamfanya
Sarai aonekane duni/asiyefaa mbele za Hajiri. Ndipo Sarai akamwambia
mumewe kusema ‘ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi
wangu kifuani mwako, naye alipoona amepata mimba, mimi nimekuwa duni
machoni pake. BWANA na ahukumu kati ya mimi na wewe’. Maandiko
hayatuelezi endapo Abramu aliwahi kumwambia mkewe kwamba unipe mjakazi
wako nimwingie ili kukuzalia mtoto. Lilikuwa ni wazo la Sarai, naam
akalitekeleza, bila kujua matokezo ya mawazo yake ni nini. Ukiendelea
kusoma Biblia utagundua kwamba jambo hili liliwakosanisha Sarai na
Hajiri, si hivyo tu lakini hata ndoa yake iliathirika. Laiti angedumu
kwenye ahadi ya Mungu, fedheha aliyoipata isingemtokea.
Ee Mwanamke, Je umeona jinsi wanandoa hawa yaani Safira, Yezebeli na Sarai
walivyotumia vibaya nafasi zao? Ni Wake wangapi leo wanafanya mambo
yanayofanana na haya kwa kujua au kutokujua? Ndoa ngapi leo zipo kwenye
matatizo kwa kuwa Wake wanawadharau waume zao? Ndoa ngapi leo
zimeharibika kwa sababu Wake hawawashauri vema waume zao juu ya Zaka na
Sadaka? Ndoa ngapi leo zimeharibika kwa kuwa Wake hawataki kuwapa waume
zao haki ya tendo la ndoa? Ndoa ngapi leo zinaharibika kwa sababu Wake
wanawaunga mkono waume zao kufanya yaliyo maovu? Naam imefika mahala
Wake wanakubali kufanya zinaa kinyume na maumbile na waume zao? Naam
ndoa ngapi leo zimeharibika kwa kuwa wanawake hawapo kwenye nafasi zao
kama Wasaidizi, Washauri, Waleta kibali na Walinzi, na hivyo Shetani anatumia uzembe wao kuharibu ndoa zao? Naam baadhi ya akina mama wanafanya mambo mabaya kwa lengo la kuwapendeza waume zao, wasijue kadri wanavyotoka nje ya nafasi zao kiroho, ndivyo adui anavyopanda uharibifu kwenye ndoa zao ili kukwamisha kusudi la Mungu kupitia ndoa zao.
Mambo ya muhimu kwa mwanamke kujua kuhusiana na nafsi ya kuwa mlinzi ni a)
Mke amepewa/amefanywa kuwa ‘Mlinzi’ wa ‘Mume’ katika ulimwengu wa roho
akali hapa duniani b) Ni wajibu wa Mke kama ‘Mlinzi’ kusimama kwenye
nafasi yake ili kuhakikisha kusudi la Mungu linafanikiwa kupitia ndoa
yake c) Ili Mungu ampe Mke taarifa kuhusu mumewe na nyumba yake, Mke
sharti awe kwenye nafasi yake maana Mungu hua anatoa taarifa kwa walinzi
tegemeana na ‘nafasi zao’ d)Mke anapsawa kuitumia ‘taarifa’ anayopewa
na Mungu kama ‘fursa’ ya uponyaji wa ndoa yake.
Wake wengi leo wamebaki kuwalaumu waume zao kutokana na mambo wanayoyafanya ili hali wao hawafanyi pia wajibu wao. Je mara ngapi kwa siku unamuombea mumeo kwa kumaanisha? Ni ulinzi kiasi gani umemuwekea mumeo? Je unafafamu kwamba suala la usalama wa mume wako, Mungu ameliweka kwako? Naam usipofanya na Yesu hafanyi? Ukinyamaza na yeye ananyamaza? Unajua kwa nini? Ni kwa sababu Mungu hawezi kuweka ulinzi juu ya mji, kama Mlinzi wa mji hajasema ‘BWANA linda mji huu’ (Isaya 62:6-7). Naam Jenga
nidhamu ya kuomba kila siku kwa ajili ya mumeo ili Mungu aachilie
ulinzi wake juu ya mumeo kwa kuwa wewe, kama Mlinzi uliyeko kwenye
nafasi, umeshauri na umeelekeza kufanya hivyo. Naam ni wajibu wako pia kutumia damu ya Yesu kumwekea mumeo ulinzi kwenye kila eneo la misha yake na hivyo kuiponya ndoa yako (Asomaye na afahamu).
Maoni