NAMNA MWANAMKE ANAVYOWEZA KUTUMIA NAFASI ZAKE KUBADILISHA MAISHA YA NDOA YAKE
SEHEMU YA NNE B
Na: Patrick Sanga
Nafasi ya tano – Mwanamke kama Mjenzi 
Katika sehemu ya 4a tulianza kwa kuangalia nafasi ya tano hata hivyo 
kutokana na urefu wake nikaona vema kuigawanya nafasi hii ya tano katika
 kipengelea a na b. Ili kusoma sehemu ya 4a bonyeza link ifuatayo https://nsanacz.blogspot.com/2018/05/namna-mwanamke-anavyoweza-kutumia_47.html Katika sehemu ya 4b tutangalia ni kwa namna gani mwanamke atapata 
hekima ya kumsaidia kujenga ndoa yake. Karibu sasa tuendelee…
Hebu tuanze kwa kuangalia mstari wa ajabu sana katika Muhubiri 7: 12 unasema ‘Kwa maana hekima ni ulinzi, kama vile fedha ilivyo ulinzi, na ubora wa maarifa ni ya kwamba hekima humhifadhi yeye aliyonayo’.
 Hekima ndio nguzo kuu ya ujenzi wa ndoa yako, naam ukiwa nayo ni 
dhahiri kwamba italeta uponyaji kwenye ndoa yako pia. Mwanamke kama 
mjenzi anahitaji kuwa na hekima ili kulinda ndoa yake akijua kwamba ki –
 nafasi yeye ni Mlinzi wa mumewe. Kumbuka kwamba andiko letu la msingi 
katika sehemu hii ya nne ni Mithali 14:1 unaosema “Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa  kwa mikono yake mwenyewe”
Je, utapataje hekima ya kuijenga ndoa yako?
Zifuatazo ni njia ambazo zitakusaidia kupata hekima ya ki – Mungu ili kujenga, kuhifadhi na hivyo kuiponya ndoa yako:
a)    Kwa kuomba 
Biblia katika Yakobo 1:5 inasema ‘Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa’. Je ni hekima ya namna gani hii? Yakobo anaendelea akifafanua kuwa ‘Lakini
 hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari 
kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, 
haina unafiki’ (Yakobo 3:17). Kisha kwenye ule mstari wa 13 anauliza ‘N’nani aliye na hekima na ufahamu kwenu? Na aonyeshe kazi zake kwa mwenendo wake mzuri, katika upole wa hekima’ (Yakobo 3:13).
Je mama umeona jinsi mistari hii inavyozungumzia hekima kwa upekee 
wake? Ni dhahiri kwamba hekima ya namna hii ikiwa ndani yako kwa 
vyovyote vile ndoa yako itajengwa kwenye msingi imara, naam unahitaji 
kuomba kwa Mungu akupe hekima safi ambayo ndani yake itajenga msingi wa 
amani, upole na kudhihirisha matunda mema. Naam kwa hekima utaonyesha 
mwenendo wako mzuri katika nyumba yako.
Naam Yesu alisema ‘aombaye hupewa…’ (Matahyo 7:7), omba ukiamini Mungu atakupa hekima hii, si
 tu kwa ajili ya uponyaji wa ndoa yako, bali kwa ajili ya kusudi lake 
kupitia ndoa yako pia. Maana kadri ndoa yako inavyokuwa na amani ndivyo 
na kusudi la Mungu kupitia ndoa yako litakavyofanikiwa.
b)   Kwa kusoma neno la Mungu
Katika Mithali 4:5,7 Biblia inasema ‘Jipatie hekima, jipatie 
ufahamu; usiusahau; Wala usiyakatae maneno ya kinywa changu. Bora 
hekima, basi jipatie hekima; Naam kwa mapato yako yote jipatie ufahamu’.
Ni muhimu sana kwako Mwanandoa ukaweka utaratibu wa kujifunza neno la
 Mungu kila iitwapo leo kwa kuwa ndani ya neno kuna hekima na ufahamu 
wakukusaidia. Biblia inasema ‘apendaye mafundisho upenda maarifa’ (Mitahli 12:1) tena katika Mithali 19:2a inasema ‘si vema nafsi ya mtu ikakosa maarifa…’
Ni vizuri ukafahamu kwamba ‘mlinzi yeyote katika ulimwengu wa 
roho lazima awe na taarifa za kutosha kuhusu lindo lake na kwa jinsi 
hiyo hiyo mwanamke kama mlinzi lazima awe na ufahamu wa kutosha wa neno 
la Mungu ili limuongoze katika kumpa hekima ya kiulinzi wa ndoa/nyumba 
yake. Naam ni LAZIMA ujijengee mazoea na nidhamu ya wewe binafsi kusoma 
neno la Mungu kila leo.
c)    Kwa kujifunza kwa waliotangulia
Katika kitabu cha Tito 2:3-5 Biblia inasema ‘ vivyo hivyo na wazee
 wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe na usingiziaji; wasiwe 
wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema ili wawatie wanawake 
vijana akili, wawapende waume zao na kuwapenda watoto wao na kuwa
 wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii 
waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe’.
Naam ni muhimu sana kujifunza kwa wanawake wenye hekima 
waliokutangulia na wenye kumjua Mungu vizuri kama Tito anavyoelekeza. 
Hii ni kwa sababu si tu kwamba utajifunza kutoka kwenye hekima yao bali 
pia kutokana na uzoefu wao binafsi wa kuwa kwenye ndoa zao. Ni dhahiri 
kwamba hata wao wamepitia/walipitia kwenye changamoto mbalimbali na kwa 
msaada wa hekima wakazijenga ndoa zao katika BWANA hata zimekuwa na 
ushuhuda mzuri na leo tunamshukuru Mungu na kujivunia akina mama ambao 
licha ya changamoto walizokutana nazo kwanza hawakutoa siri za ndoa zao,
 pia kwa hekima walijifunza kuvumilia, wakatafuta amani, wakasamehe 
waume zao na kwa jinsi hiyo jina la BWANA halikutukanwa. Naam watafute 
hao ujifunze kwao maana hata leo wanapatikana.
d)   Kwa kuokoka
Wanawake wengi sana ambao ni wanandoa, ndoa zao zinashida kwa sababu 
Yesu si BWANA kwenye ndoa zao. Ili Yesu afanyike BWANA sharti wokovu 
uingie kwenye nyumba yako, kwa kuamua kuokoka. Najua jambo hili linaweza
 likaleta shida kwa wewe ambaye umeokoka, ukajiuliza mbona nimeokoka 
lakini bado ndoa yangu ina shida, naam mosi angalia hizo nafasi nyingine
 uzifanyie kazi, lakini pili mruhusu Yesu afanyike BWANA (Mtawala, Kiongozi, Mshauri) wa ndoa yako.
 Endapo utaokoka na kuenenda vema katika kuukulia wokovu uwe na uhakika 
yeye ni Mponyaji, na uponyaji wake hauna mipaka, naam unaweza 
kumkaribisha akusaidie kuiponya ndoa yako.
Ukisoma Biblia katika Wakolosai 2:3 biblia inasema ‘ambaye ndani yake yeye (Yesu Kristo) hazina za hekima na maarifa zimesitirika’ Maneno ndani yake yeye ndiyo ninayotaka uyaone kwa upana katika mstari huu. Andiko hili linafanya tujue kwamba ziko hekima za namna mbalimbali kutoka kwa BWANA ambazo tunazihitaji ikiwa ni pamoja na hekima ya kujenga nyumba/ndoa yako.
 Naam ili hekima ipate nafasi ya kuponya ndoa yako sharti mwenye hekima 
si tu apate nafasi ndani yako bali afanyike BWANA na mwokozi wa maisha 
yako kwenye maisha yako. 
Hebu tuangalie mifano kadhaa:
Mfano wa Mke wa Nabali
Ukisoma Biblia katika kitabu cha 1Samweli 25:2-35 utaona habari za 
mtu aliyeitwa Nabali ambaye alitaka kuleta maafa na msiba mkubwa kwenye 
nyumba yake kwa kitendo cha kuwatukana Daudi na watu wake, licha ya 
Daudi kufanya kazi kubwa ya kulinda mifugo ya Nabali ilipokuwa 
mashambani dhidi ya Wafilisti. Kutokana na dharau ya Nabali, Daudi 
aliapa kwenda kumuangamiza Nabali pamoja na nyumba yake yote. Maandiko 
yanasema Mke wa Nabali aitwaye Abigaili alipopata taarifa ya 
yalitokea alifanya hima kwa hekima kumsihi Daudi amsamehe mumewe kwa 
upumbavu alioufanya, naam na kwa neno la Abigaili Daudi alisamehe.
Tunajifunza nini? 
Abigaili alizijua nafasi zake vema kama mke kwa mumewe na hivyo 
alizitumia nafasi zake kuiponya ndoa yake. Je, umeshawahi kufikiri kwa 
nini Mtumishi wa Nabali alienda kumpa taarifa Abigaili ya uovu ambao 
mumewe amewatenda watumwa wa Daudi? Biblia inasema yule Mtumishi 
alimweleza hivi Abigali ‘Basi sasa ujue na kufikiri utakavyotenda; 
kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya Bwana wetu (Nabali), na juu ya 
nyumba yake yote, kwa kuwa yeye ni mtu asiyefaa kabisa, hata mtu hawezi 
kusema naye’ (1Samweli 25:17).
Hii ni kwa sababu Abigaili alikuwa Mlinzi wa Nabali na kwa kuwa alikuwa kwenye nafasi zake, taarifa za msingi juu ya lindo lake zilimtafuta.
 Naam mwanamke aliyesimama kwenye nafasi zake hakuna jambo litatokea au 
linalokuja mbeleni litatokea bila yeye kuwa na taarifa, na ndio maana 
Mungu anataka ujifunze mambo haya.
Baada ya Abigaili kupata taarifa husika, aliandaa chakula na kwenda 
kwa Daudi kuomba msamaha kwa ajili ya mumewe na  Daudi alijibu hivi …
 Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli ambaye amekuleta hivi leo 
kunilaki, na ibarikiwe busara yako, na ubarikiwe wewe, uliyenizuia hivi 
leo nisimwage damu, wala kujilipiza kisasi kwa mkono wangu mwenyewe (1Samweli 25:32-33).
Je umeliona jambo hili lakini? naomba rudia tena kusoma maneno ya 
Daudi hapo juu. Naam umeshawahi kujiuliza kwa nini Daudi aanze kumhimidi
 Mungu kutokana na kitendo cha Abigaili? Kwa lugha rahisi Daudi alikuwa 
akisema ‘atukuzwe Mungu aliyempa Nabali mke mwenye Busara/hekima kiasi 
hiki’ (Mithali 19:11), maana kwa busara ya huyu mama nimezuiliwa 
nisimwage damu’. Naam Daudi hakuishia tu kumbariki Mungu bali alimbariki
 na Abigaili akasema ‘Na ibarikiwe busara yako naam na ubarikiwe wewe 
Abigaili’ kwa kuchagua kuwa mwanamke mwenye hekima nk.
Tambua kwamba, kama si Abigaili kusimama kwenye nafasi zake, 
siku ile si tu Nabali angekufa bali yote yaliyokuwa chini yake 
yangeharibiwa na kutekwa pia. Pengine Biblia ingeandika matukio 
yote ya Nabali ungeshuhudia namna ambayo mkewe alitumia hekima yake 
kuilinda na kuijenga ndoa yake. Ni imani yangu kila mumewe
 alipotenda kwa uovu, mkewe kwa hekima kama mjenzi alitengeneza ndoa 
yake kama alivyofanya na kwa Daudi, naam kwa nafasi yake Abigaili alizuia msiba usiingie katika nyumba yake.
Hata leo wapo akina mama wengi sana ambao wanamlilia Mungu aziponye 
ndoa zao kwa sababu zina shida kubwa. Katika hao wanaomlilia Mungu, si
 wote wanaojua kwamba Mungu anafanya kazi kwa taratibu na kanuni 
alizojiwekea. Ni matarajio ya Mungu kuona kila Mwanamke aliyeko kwenye 
ndoa anasimama kwenye nafasi zake, kutokea kwenye nafasi zake ndipo 
Mungu atasema na kumuongoza huyo mama juu ya nini cha kufanya ili 
kuponya ndoa yake na si vinginevyo.
Kumbuka kwamba ‘ni vigumu sana kwa Mungu kukusaidia/kukupigania kama hauko/haujasimama kwenye nafasi zako’.
 Katika kufanya kazi zake hapa duniani Mungu anaangalia nafasi ambazo 
amewapa watu kwenye ulimwengu wa roho. Naam wale ambao wapo kwenye 
nafasi zao ndio ambao Mungu anafanya nao kazi. Hivyo sio suala la kulia 
tu, bali ni suala la kusimama kwenye nafasi yako kama Mjenzi wa ndoa 
yako na utaona mabadiliko makubwa sana. Kumbuka pia na adui naye akitaka
 kuharibu ndoa yako sharti akuondoe kwenye nafasi zako, hii ni kuonyesha
 kwamba nafasi alizokupa Mungu kwenye ulimwengu wa roho zina thamani 
kubwa sana.
Mfano wa Stefano 
“Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, 
na la Wakirene, na la Waiskanderia, na wale wa kilikia na Asia 
wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na 
hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye” (Matendo ya Mitume 6: 9 
-10). Naamini umeliona jambo hili wewe mama, jaribu kufikiri watu kutoka
 kwenye masinagogi matano tofauti walikuwa wakishindana na Stefano kwa 
habari za Injili aliyowashuhudia. Utamu wa habari hii ni kwamba 
Stefano alishinda na zaidi ya kushinda kwa sababu mosi, si tu alijazwa 
Roho Mtakatifu, bali kwa sababu ndani yake kulikuwa na hekima ambayo 
ilipita fahamu za wapinzani wake wote. Naam hivi ndivyo hekima ilivyofanyika ulinzi kwa Stefano na kwa shauri la BWANA.
Binafsi nalipenda sana andiko hili, maana linadhihirisha uwezo wa hekima katika kutenda, kulinda, kuhifadhi, kuponya nk. Naam
 si tu Roho Mtakatifu alimsaidia Stefano bali pia hekima aliyokuwa nayo 
Stefano ilimjengea mazingira mazuri Roho Mtakatifu ya kumshindia Stefano.
 Hekima hii ndiyo iliyokuwa ndani ya BWANA wetu Yesu Kristo alipokuwa 
bustanini na wanafunzi wake, wakati wa mateso yake na hata kifo chake. 
Maana alisema ‘Baba uwasamehe maana hawajui walitendalo’.  Mpenzi msomaji fikiri endapo ungekuwa wewe kwenye mazingira kama ya Stefano au Yesu ungechukua uamuzi gani?
Nimeandika Mfano huu wa Stefano si kwa bahati mbaya bali kwa kusudi 
kamili. Najua kesi ya Stefano haikuwa ya ndoa, bali upinzani dhidi ya 
injili ya Kristo. Nilichotaka kukuonyesha ni uwezo wa hekima katika 
kulinda, kuhifadhi, kusaidia nk wakati mtu anapokutana na changamoto 
mbalimbali. Hekima ya Mungu ilimsaidia Stefano kutokana na mazingira 
yake, naam na hata kwako inaweza kukusaidia kuiponya ndoa yako. Naam 
hekima ni Mlinzi, hekima ni Mjenzi, hekima ni Mponyaji nk, kwa neema ya 
Mungu, kupitia ujumbe huu nimemtambulisha Hekima kwako mama, MTAFUTE NA 
KUMTUMIA ATAKUSAIDIA KUIPONYA NDOA YAKO. 
Ahsante kwa kufuatilia mfululizo huu, katika sehemu ya tano (5) 
nitaweka sehemu ya mwisho ya ujumbe huu muhimu kwa wanadoa… naam usiache
 kuomba kwa ajili yangu.
Utukufu na Heshima vina wewe Yesu! Wastahili BWANA wetu.





Maoni