NAMNA MWANAMKE ANAVYOWEZA KUTUMIA NAFASI ZAKE KUBADILISHA MAISHA YA NDOA YAKE
Na: Patrick Sanga
Mithali 14: 1 ‘Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe’.
Mchungaji mmoja rafiki yangu aliniambia asilimia hamsini mpaka sabini
ya changamoto au matatizo anayoshughulika nayo mara kwa mara katika
kanisa lake ni ya wanandoa. Kwa lugha nyepesi asilimia 50 – 70 ni
matatizo yatokanayo au yanayohusiana na ndoa. Binafsi pia kwa upande
wangu kupitia nafasi yangu katika mwili wa Kristo, email za wasomaji
ninazopata na pia baadhi ya semina za ndoa ambazo nimefanya kuhusu eneo
hili nimegundua kwa hakika ndoa nyingi za wana wa Mungu zina shida na
wao hawajajua kwamba vita hii inatoka kwa Shetani, maana anajua ndoa
zikitengamaa ni faida kwa ufalme wa Mungu na ni uharibifu kwenye ufalme
wake wa giza. Naam anapigana usiku na mchana ili kuhakikisha ndoa
hazitengamai kwa kuleta fujo za kila aina.
Kila siku katika ndoa kuna changamoto zinazaliwa mpaka imefika mahala
baadhi ya wanandoa wanawaza kwa nini walikubali kuoa au kuolewa. Kwa
hakika laiti Biblia ingetoa mwanya kwa wanandoa kuachana basi kuna
baadhi ya wanandoa wangehakikisha wanaitumia hiyo nafasi vizuri kwa kuwa
ndoa zimegeuka ndoano. Matarajio ambayo kila mmoja alikuwa nayo kwenye
ndoa anaona hayatimii. Kinachosumbua watu wengi ni kwamba kabla
hawajaonana hawakujua nini kinakuja kupitia ndoa, hawakuweza kuona
uhalisia wa maisha ya ndoa utakuwaje? Bali kila mmoja alikuwa na
mtazamo/fikra na matarajio yake binafsi juu ya ndoa yake.
Naam zipo sababu nyingi sana zinazopelekea matatizo au changamoto kwa
wanandoa. Katika somo hili nitaandika zaidi zile zinazotokana na
upinzani kutoka kwa Shetani ili kuathiri kusudi la Mungu. Lengo la
ujumbe huu ni kukufundisha wewe mama (Mwanandoa) namna ya kuzitumia
‘nafasi’ ambazo Mungu amekupa Kibiblia ili kuiponya ndoa yako au
kubadilisha hali ya sasa ya ndoa yako endapo unaona si ile ambayo Mungu
amekusudia.
Kwa nini Mwanamke?
Pengine utaniuliza kwa nini mwanamke ndiye awajibike katika kuponya
au kubadilisha maisha ya ndoa yake? Binafsi katika kuisoma Biblia
nimegundua kwamba kwa kuzingatia nafasi ambazo mwanamke amepewa kibiblia
ni ishara ya kwamba kwa habari ya ndoa, Mwanamke ana nafasi kubwa ya
kuijenga au kuibomoa ndoa yake na hivyo nyumba yake kwa ujumla. Mara kwa
mara Mungu ananifundisha masuala ya wanawake, suala la wanawake kuwa
kwenye ‘nafasi zao’ husisitizwa sana.
Kwa nini nafasi?
Sijui kama unafahamu maana ya nafasi ambayo Mungu anampa mtu katika
ulimwengu wa roho. Hizi ni nafasi ambazo Mungu amekupa wewe mawanamke
katika ulimwengu wa roho ili uzitumie kufanikisha kusudi lake kupitia
ndoa yako. Nafasi (position) ni eneo ambalo mtu anapaswa kuwepo kwa
kuhusianisha na vitu au watu wengine, naam ni wadhifa ambao mtu anakuwa
nao kwa kuhusianisha na mtu au watu wengine.
Kwa hiyo hizi ni nafasi ambazo Mungu amempa mwanamke zikihusiana na
mwanaume katika kilitumika kusudi la Mungu hapa duniani. Mwanamke
anapokuwa amesimama katika nafasi zake ndipo anapoweza kuruhusu mawazo
ya Mungu kupitia ndoa yake kutimia naam ndivyo anavyoweza kuzuia mawazo
ya Iblisi kupitia ndoa yake yasitimie. Naam nafasi ya mwanamke katika
ndoa ndiyo inayoamua uzima au mauti ya ndoa yake, nafasi ndiyo
inayopelekea kufanikiwa au kufeli kwa ndoa yake, nafasi ya mwanamke
katika ndoa ndio inayoamua nini kingie au kitoke kwenye ndoa.
Katika kusoma kwangu Biblia nimegundua kwamba Mungu amempa nafasi zifuatazo mwanamke;
- Mwanamke kama ‘msaidizi’ wa mumewe
- Mwanamke kama ‘mlinzi’ wa mwanaume
- Mwanamke kama ‘mjenzi’ wa nyumba yake
- Mwanamke kama ‘mshauri’ wa mumewe
- Mwanamke kama ‘mleta kibali’ kwa mumewe
Naam kutokana na changamoto zinazoendelea katika ndoa mbalimbali
nimelazimika kuanza kuandaa mfululizo huu wa namna mwanamke anavyoweza
kusimama kwenye nafasi zake na kuiponya ndoa yake. Jukumu langu kubwa
itakuwa ni kufafanua kila nafasi ambayo mwanamke amepewa na namna
anavyoweza kuitumia hiyo nafasi kubadilisha ndoa yake ambayo anaona
inaangamia.
Maoni