NAMNA MWANAMKE ANAVYOWEZA KUTUMIA NAFASI ZAKE KUBADILISHA MAISHA YA NDOA YAKE (Part 2)
Na: Patrick Sanga
Maada: Nafasi ya Msaidizi, Mshauri na Mleta kibali
Ili kusoma sehemu ya kwanza bonyeza link hii https://nsanacz.blogspot.com/2018/05/namna-mwanamke-anavyoweza-kutumia.html
Mpenzi msomaji, Mungu akubariki kwa kufuatilia mfululizo wa somo
hili. Ni imani na maombi yangu kwamba masomo haya yatafanyika msaada
kwenye maisha yako na ndoa yako kwa ujumla. Katika sehemu hii ya pili
nitaandika kuhusu nafasi tatu ambazo ni nafasi ya Mwanamke kama Msaidizi, Mshauri na Mleta kibali.
Mwanamke kama Msaidizi
Mwanzo 2:18 ‘BWANA Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye’. Ukisoma mstari huu katika toleo la GNB Biblia inasema ‘Then the LORD God said, “It is not good for the man to live alone. I will make a suitable companion to help him.”
Biblia inatueleza kwamba Adam ndiye aliyetangulia kwanza kudhihirishwa
kabla ya Mwanamke. Kabla ya Hawa kuletwa, Mungu alimpa Adam majukumu
mengi ambayo alipaswa kuyatekeleza.
Katika kutekeleza majukumu yake Adam aliona kwamba amepungukiwa
mwenza wa kufafanana naye na ndani yake akatamani angepata mtu wa kuwa
naye karibu kwa kila afanyalo. Ukweli huu tunaupata tukisoma Mwanzo 2:20
kwamba ‘Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na
ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa
kumsaidia Adamu aliyefanana naye. Naam kutokana na upweke wa
Adam ndipo Mungu akamfanya Hawa mkewe kama msaidizi. Kitendo cha Mungu
kumfanya mwanamke kama msaidizi ni ishara kwamba Mungu alijua kuwa Adam
hawezi kuwa na ufanisi mzuri katika kutekeleza majukumu (Kusudi)
aliyopewa bila mwenza wa kufanana naye.
Maandiko yanasema kwamba ‘Maana mwanaume hakutoka katika
mwanamke, bali mwanamke katika mwanaume. Wala mwanaume hakuumbwa kwa
ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanaume’
(1Wakorinto 11:8-9). Ile kwamba mwanamke aliumbwa kutoka kwa mwanaume
na kwa ajili ya mwanaume ni kuonyesha kwamba wajibu au nafasi mojawapo
ya mwanamke ni kuwa msaidizi wa mumewe. Hata hivyo neno msaidizi
halipaswi kutafsiriwa vibaya na kuonyesha kwamba mwanamke hana thamani.
Mwanamke ni msaidizi wa mume katika kulitumikia kusudi la Mungu
isipokuwa kinacho watofautisha ni utendaji wao tu. Mume hapaswi
kumdharau mkewe wala mke kumdharau mumewe kwa kuwa mume si mume bila mke
na mke si mke bila mume, wao ni mwili mmoja, kusudi lao ni moja na
BWANA wao ni mmoja. Maandiko yafuatayo yanaonyesha baadhi ya mambo
ambayo mwanamke anapokuwa katika nafasi ya Msaidizi anapaswa kuyafanya;
Tito 2:4 inasema ‘Ili wawatie wanawake vijana akili,
wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao, na kuwa wenye kiasi, kuwa
safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe;
ili neno la Mungu lisitukanwe’.
1 Timotheo 5: 14 ‘Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, wawe na madaraka ya nyumbani; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu’. Ukisoma pia katika 1 Wakorinto7:4a kwa habari ya tendo la ndoa Biblia inasema ‘Mke hana amri juu ya mwili wake…’ na mstari wa 5a unasema’ Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda…,
Naam hii ina maana kama mke ataweka amri kwa habari ya tendo la ndoa
kwa mumewe ajue kabisa ameshindwa kumsaidia mumewe na kuna hatari ya
kuanguka kwenye zinaa. Naam Mungu anataka akina mama walioko kwenye ndoa
wajifunze kuwasaida waume zao wasiingie kwenye zinaa.
Naam hata sasa ni muhimu sana wewe mama ukajua Mungu amewaunganisha
ili kufanya nini hapa duniani kwa ajili ya ufalme wake. Changamoto kubwa
iliyipo leo ni kwamba wanandoa wengi wameingia kwenye ndoa kwa sababu
ni desturi ya wanadamu kuoa na kuolewa. Wengi wameshindwa kuunganisaha
suala la kuoa au kuolewa na kumtumikia Mungu kupitia ndoa yao. Mungu
anapokuunganisha na mumeo maana yake anakupeleka kwenye wajibu wa kuwa
msaidizi kwa mumeo. Naam hakikisha kwamba unafanyika msaada kwa mumeo
kwa namna ambayo kile ambacho mnajua kwamba Mungu amewapa kukifanya hapa
duniani kinafanikiwa. Zaidi unaweza soma Mithali 31:10-31 ili kuongeza
ufahamu zaidi kuhusu nafasi ya mwanamke kama Msaidizi.
Mwanamke kama Mshauri
Katika hali ya kawaida watu wengi hutafsiri mshauri kuwa msiaidizi.
Kwa kuzingatia dhana ya nafasi katika ulimwengu wa roho imenilazimu
kutenganisha ili kukuonyesha umuhimu wa nafasi ya mwanamke kama Mshauri.
Biblia katika Mithali 31:26 inasema ‘Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema i katika ulimi wake’.
Naam andiko hili linatupa kujua kwamba Mke ndiye mshauri mkuu wa
mumewe. Siri moja ya mwanamke kuwa mshauri mzuri ni kuwa na ufahamu wa
kutosha wa neno la Mungu. Hivyo kama Mke hana hekima itokanayo na neno
la Mungu kwa wingi ndani yake, hawezi kuwa mshauri mzuri. Ushauri
unategemea nguvu za ufahamu alizonazo Mwanamke, kadri anavyokuwa na
ufahamu wa kutosha wa neno ndivyo anavyokuwa kwenye nafasi ya kutoa
ushauri bora kwa mumewe.
Biblia katika kitabu cha Mithali 8: 14-16 inasema ‘Shauri ni
langu, na maarifa yaliyo sahihi; Mimi ni ufahamu na mimi nina nguvu. Kwa
masada wangu wafalme humiliki, Na wakuu wanahukumu haki. Kwa msaada
wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia’.
Fahamu kwamba hekima ndani yako mama itakupa maarifa na ufahamu wa
kumshauri mumeo ili kufanya maamuzi sahihi katika kila atendalo. Hekima
ni sawasawa na shauri/maarifa/ufahamu/nguvu. Ukiona kiongozi yoyote
anatawala/anaongoza watu vizuri ujue washauri wake wanamshauri vizuri au
ujue ana wahsauri wazuri. Vivyo hivyo mwanaume anafanya kazi zake vema
na kufanikiwa katika yale atendayo ujue nyuma yake kuna mwanamke mwenye
nguvu za ufahamu anayemshauri vema.
Naam chanagmoto au matatizo mengi yaliyopo kwenye ndoa leo ni matokeo
ya akina mama kukosa hekima itokanayo na neno la Mungu ya kuwashauri
waume zao. Wengi wanategemea akili zao, au ushauri wa rafiki zao nk.
katika kuangalia ndoa zao na mambo yao yaendaje. Kutegemea ushauri wa
watu wengine bila wewe mwenyewe mama kutafuta hekima itokanyo na Mungu
kwanza inaweza kukufikisha kupata ushauri wa kipepo kama ilivyomtokea
Hawa pale Bustanini. Kumbuka Mshauri ni mtoa taarifa, mtoa pendekezo juu
ya nini mume wake aweza fanya au kutofanya.
Mwanamke kama mleta kibali.
Hii ni nafasi ya ajabu sana ambayo Mungu amempa mwanamke. Mwanamke
anapokuwa kwenye hii nafasi mambo matatu yanafanyika; 1) Mume anaingia
kwenye ngazi ya kushirikishwa siri/mambo/majukumu mengi kutoka kwa
BWANA. 2) Kukubalika kwa mume wake katika jamiii/kazi/kanisa nk
kunaongezeka 3) Na mwisho maombi ya mume wake yanasikilizwa. Mambo haya
yanathibitishwa na Biblia katika Mithali 18:22 inayosema ‘Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa BWANA’, pia Mithali 31: 23 inayosema ‘Mume wake hujulikana malangoni; Aketipo pamoja na wazee wa nchi’
Zaidi kwa habari ya maombi ya mume kusikilizwa au kutokusikilizwa Biblia katika 1 Petro 3:7 inasema
‘Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke
heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema
ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe’. Naam hii ni ishara
kwamba mke anaweza kusababisha maombi ya mumewe yakasikilizwa au
yasisikilzwe. Unaweza ukafikiri hili andiko linawahusu akina baba pekee,
lakini ukilitafakari kwa upana utagundua kwamba linawahusu akina mama
pia ili wajue kwamba kuwa mke ni nafasi ambayo inaweza
kuzuia maombi/baraka/majibu au kukwamisha mafanikio ya waume zao kama
hawatukuwa makini katika kuwasaidia waume zao kuishi nao kwa akili.
Si wengi wanaojua kwamba kuna maombi mengi ya familia/waume zao
hayajibiwi kwa sababu maombi ya mume ambaye ndiye kichwa hayasikilizwi
na Mungu. Na chanzo cha kutokusikilizwa ni kuharibika kwa uhusiano kati
ya mume na ‘mleta kibali’ wake yaani mke. Hivyo wewe mama mwenye ufahamu
huu jifunze kwenda mbele za Mungu na kuomba toba kwa ajili ya mumeo
mara kwa mara. Kwa sababu kuna vitu au maamuzi anayoweza kufanya nay eye
akaona yuko sahihi lakini kumbe ni uamuzi ambao unajenga ukuta kati ya
maombi yake na Mungu wako.
Hakikisha unasimama vema kwenye hii nafasi ili Mungu alete
uponyaji kwa mume wako na maombi yake yaweze kusikilizwa. Naam simama
kwenye nafasi yako ili kumjengea mazingira mazuri mumeo ya kuishi na
wewe, ndivyo na maombi yake yatakavyosikilizwa, ndivyo atakavyopata
kibali mbele za BWANA, naam atakuwa mume bora katika jamii na kufanikiwa
katika kila atendalo.
Tamati endapo mwanamke atakaa vizuri kwenye nafasi hizi haijalishi
mume wake ni mgumu kiasi gani, mama akizungumza kwa maana ya maonyo au
ushauri lazima mwanaume asikilize au kufuata kile ambacho msaidizi,
mlinzi, mleta kibali wake nk anamweleza, na kama akikataa uharibifu ni
haki yake. Mungu ameweka sauti ndani ya mwanamke ambayo inaweza kuleta
uponyaji kwa mumewe endapo mwanamke atakaa vizuri kwenye hizi nafasi.
Maoni